MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma MheshimwaJulius Mtatiro,amewaagiza viongozi wa vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos)na idara ya Ushirika Halmashauri ya wilaya Tunduru kuhakikisha wanadhibiti utoroshaji wa zao la mbaazi na kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuwasaidia wakulima waweze kujiinua kiuchumi.
Mtatiro amesema hayo , wakati akizungumza na mameneja na wenyeviti wa Amcos,maafisa tarafa na viongozi wa Chama kikuu cha Ushirika(Tamcu katika kikao cha maandalizi ya makusanyo ya zao hilo na mazao mchanganyiko kwa msimu wa masoko 2023/2024.
“Mwaka jana kulikuwa na ucheleweshaji kutokana na watu wa mifumo kuchelewa kufanya uzembe hali iliyopelekea kuchelewa kuanza msimu wa makusanyo na ununuzi wa mbaazi,mwaka huu sitaki kusikia hali hiyo inajitokeza tena”alisema.
Aidha alisema,zao mbaazi katika msimu 2023/2024 litaendelea kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kuwaonya wakulima,viongozi,watunza maghala na wanunuzi wanaokusudia kuharibu mfumo huo ambao umeonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima.
Amewataka viongozi wa vyama na bodi za Ushirika wilayani humo,kuwa waaminifu na kuepuka kujihusisha na ubadhirifu,bali wahakikishe wanaongoza vyama hivyo kwa kufuata taratibu na sheria za vyama vya Ushirika.
“hakutakuwa na huruma kwa yoyote atakayejaribu kuvuruga ununuzi wa mbaazi katika msimu wa mwaka huu,nawaombeni sana viongozi wenzangu twendeni tukawasaidia wakulima wetu huko vijijini”alisisitiza Mtatiro.
Amewataka wakulima,kutokubali kudanganywa na wafanyabiashara wanaopita kwenye maeneo yao kwa ajili ya kuhitaji kununua mbaazi nje ya mfumo huo kwa bei ndogo isiyolingana na gharama za uzalishaji na kueleza kuwa,serikali imejipanga kuwashughulikia watu hao.
Alisema,mfumo wa soko huria ni wa kinyonyaji na hauna nafasi tena katika wilaya hiyo kwa kuwa ndiyo uliosababisha wakulima wa mikoa ya kusini kuendelea kuwa maskini kwa muda mrefu licha ya jitihada kubwa wanazofanya mwaka hadi mwaka.
Alisema,dhamira ya serikali ni kuona sekta ya kilimo inawanufaisha wakulima kwa kupata fedha zinazostahili na serikali inapata ushuru ambao utakwenda kutumika kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma muhimu za kijamii.
Mtatiro,amewaasa viongozi na watendaji wa sekta ya ushirika kuhakikisha wanakutana na wakulima ili kuwaeleza faida za ushirika na maafisa ugani kuwatembelea kwenye shughuli zao mara kwa mara ili kuwapa ushauri wa kilimo cha kisasa na chenye tija kwa kuwa wakulima wakisimamiwa vizuri watazalisha kwa wingi na AMCOS zitapiga hatua kubwa ya kiuchumi.
Afisa ushirika wa wilaya hiyo George Bisan alisema,msimu wa mwaka 2020/2021 na 2021/2022 changamoto kubwa ilikuwa utoroshaji wa zao la mbaazi kwenye vijiji vinavyopakana na mikoa jirani ambayo hakuwa mfumo huo.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa TAMCU Iman Kalembo alieleza kuwa, katika msimu 2022/2023 Chama kikuu kwa kushirikiana na vyama vya Ushirika vya msingi viliweka malengo ya kukusanya kilo milioni 5,451,000.
Hata hivyo alisema kuwa,kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao walifanikiwa kukusanya kilo milioni 3,035,692 ambazo ni pungufu kwa kilo milioni 2,415,308 sawa na anguko la asilimia 44.31 ya lengo.
Kalembo alieleza kuwa,mbaazi ziliuzwa kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na jumla ya minada sita ya mauzo ilifanyika ambapo bei ya wastani ilikuwa Sh. 898.25 na jumla ya kilo 3,035,692 ziliuzwa zenye thamani ya Sh.bilioni 2,633,233,690.00.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.