Na Albano Midelo,Songea
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 760 katika vituo 18 vya kutolea huduma za afya mkoani Ruvuma.
Hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba hivyo kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imefanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
Akizungumza kwenye hafla hiyo mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema vifaa tiba hivyo vitasambazwa katika vituo 18 vya kutolea huduma za afya kwa awamu mbili ambapo katika awamu ya kwanza itahusisha usambazaji wa vitanda vya hospitali,magodoro na mashuka.
Amesema vifaa hivyo vinasambazwa na MSD Kanda ya Iringa na Mtwara kuanzia Machi 6,2024 kwenye vituo vilivyopo katika majimbo ya uchaguzi na Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma.
“Ni Dhahiri kabisa ujio wa vifaa tiba hivi utasaidia kuboresha huduma za afya ,tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa katika sekta ya afya’’,alisema RC Thomas.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Louis Chomboko amesema vifaa tiba hivyo vimeletwa na serikali kwa mwamvuli wa majimbo tisa ya uchaguzi mkoani Ruvuma ili kuimarisha afya za wananchi hatimaye waweze kushiriki vema katika shughuli za maendeleo.
Hata hivyo amesema kutolewa kwa vifaa hivyo ni sehemu tu ya vifaa tiba kwa sababu serikali bado inaendelea kuleta dawa na vifaa tiba kupitia MSD ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi sasa Mkoa wa Ruvuma umepokea shilingi bilioni 2.9 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini Benaya Kapinga akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Ruvuma, amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuleta vifaa hivyo ambavyo amesema vimeleta faraja kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Komred John Haule amesema wataendelea kumpongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa anafanya vitu vinavyoonekana kwa wananchi.
Amewaasa watumishi wa afya mkoani Ruvuma kuhakikisha kuwa vifaa hivyo wanavitunza na vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa
Ofisi ya Rais TAMISEMI imenunua vifaa tiba mbalimbali kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika majimbo 214 nchini yakiwemo majimbo tisa ya Mkoa wa Ruvuma
Kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Louis Chomboko akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kuhusu vifaa tiba vilivyopokewa mkoani humo kwa ajili ya majimbo tisa ya uchaguzi ambavyo vitatumika kwenye vituo 18 vya kutolea huduma za afya
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.