Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amefanya ziara ya pili ya kukagua maeneo ya mipakani kwa kutembelea mpaka wa Chiwindi mwambao mwa ziwa Nyasa unaogawa Tanzania na nchi ya Msumbiji.
RC Ibuge katika ziara hiyo aliongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Ruvuma pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Nyasa.
Akizungumza na viongozi na watendaji wa serikali katika kijiji cha Chiwindi,wilayani Nyasa,RC Ibuge ameagiza ulinzi na usalama katika eneo la mpaka kuimarishwa zaidi ili wananchi wanaoishi mpakani wasiwe na hofu bali waendelee kushiriki katika kazi za uzalishaji mali.
Hata hivyo amewataka wananchi wanaoishi mpakani kuwa walinzi wa kwanza na endapo wataona dalili za hatari wasipuuze, bali watoa taarifa haraka katika ngazi za juu ili hatua zichukuliwe haraka.
Ametoa rai kwa wananchi na wafanyabiashara wanaovuka mpaka kwenda Msumbiji kufuata maelekezo ya serikali,na hasa kutokana na kile ambacho kinaendelea katika nchi ya Msumbiji vikiwemo vitendo vya ugaidi ambapo amesisitiza kipaumbele cha kwanza kiwe ni maslahi ya Taifa.
Amewatahadharisha viongozi na watendaji waliopo mpakani wasiruhusu vitendo ambavyo vinahatarisha amani katika mipaka ya nchi ukiwemo mpaka wa Chiwindi ambako kuna mwingiliano wa wageni kutoka Msumbiji na kuingia Tanzania.
“Mipango ya serikali ni mikubwa,Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan ana lengo la kuiendeleza nchi hii ipige hatua kubwa katika maendeleo’’,alisisitiza RC Ibuge.
Hata hivyo amesema bila amani na utulivu hakuna maendeleo,ambapo amewapongeza wananchi mwambao mwa ziwa kwa kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo cha zao la muhogo.
Hata hivyo amesema serikali kupitia ngazi ya wilaya ya Nyasa, inaandaa mpango kuviwezesha vikundi vidogo ili viweze kufanya kilimo cha ziada cha kuongeza kipato ambapo amesema wilaya ya Nyasa inafaa kwa kilimo cha michikichi ambacho kinazalisha mafuta ya kula ambayo yana soko kubwa hapa nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa ziara hiyo,ambayo amesema imeleta faraja kubwa kwa wananchi wa kijiji cha Chiwindi kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.
Hii ni ziara ya pili ya RC Ibuge kukagua maeneo ya mipaka katika Mkoa wa Ruvuma,ambapo katika ziara ya kwanza RC Ibuge alikagua mpaka wa Mkenda unaoigawa Tanzania na Msumbiji kupitia Mto Ruvuma wilaya ya Songea.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 13,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.