WANAFUNZI wa shule kongwe ya Sekondari Kigonsera iliyopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,wameaswa kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo ili waweze kutimiza ndoto zao.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,wakati akizungumza na wanafunzi hao alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kuwapa hamasa na kuwakumbusha wajibu wao wa kusoma kwa bidii.
Alisema, ni vyema wanafunzi kutambua umuhimu wa elimu hivyo wanatakiwa kujituma,kuongeza bidii darasani na kusikiliza wanayofundishwa na walimu wao kama wanahitaji kufanikiwa katika maisha pindi watakapomaliza masomo yao.
“Kigonsera Sekondari ni shule nzuri na inayofanya vizuri kwa hiyo msiivunjie heshima, apa kuna miundombinu mizuri inayofaa kwa wanafunzi kujisomea nawaomba sana muitendee haki,nyinyi ndiyo wakuu wa mikoa na Majenerali wa baadaye”alisema Brigedia Jenerali Ibuge.
Alisema,Serikali imekuwa inatoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha miundombinu ya shule hiyo, na itaendelea kufanya hivyo ili kuwawekea wanafunzi mazingira mazuri ya kujisomea na walimu kuwa na mahala pazuri kwa ajili ya kufundishia.
Alisema,kila wanapolala na kuamka lazima wakumbuke jambo lililowapeleka shuleni sambamba na kuwa na malengo ambapo kupitia elimu wanayoipata darasani itawasaidia kupata ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kumudu ushindani katika soko la ajira.
Aidha Ibuge,amewataka wanafunzi hao kuwa wazalendo kwa nchi yao na kujiepusha kuiga tabia na tamaduni za kigeni zinazokwenda kinyume na maadili ya Kitanzania.
Shule ya Sekondari Kigonsera ni miongoni mwa shule kongwe apa nchi ambayo kwa nyakati tofauti imetoa viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjemin Mkapa na Waziri Mkuu wa sasa Kassim Majaliwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.