MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema Mkoa wa Ruvuma una ziada ya chakula tani 877,048 na kwamba Mahitaji ya chakula katika Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka 2020 ni tani 469,172 ikilinganishwa na uzalishaji wa mazao ya chakula ni tani 1,346,220.
Mndeme alikuwa anazungumza kwenye Mkutano wa 14 wa Baraza la wafanyakazi wa TANROADS kitaifa ambao umefanyika kwa siku mbili mjini Songea mkoani Ruvuma kwenye ukumbi wa Parokia ya kanisa katoliki la Bombambili na kufunguliwa na mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele.
Akizungumza kwenye mkutano huo ulioshirikisha wajumbe 103 kutoka mikoa yote nchini,Mndeme amesema Mkoa wa Ruvuma umeshika nafasi ya kwanza katika uzalishaji wa mazao ya chakula nchini katika msimu wa kilimo 2018/2019,ambapo amewataka wajumbe wa mkutano huo wakiwa Ruvuma wale kwa sababu Mkoa una chakula cha kutosha ukiwemo ugali,wali,maharage na samaki watamu kutoka ziwa Nyasa.
Amezitaja Takwimu za uzalishaji wa mahindi mkoani Ruvuma katika msimu wa mwaka 2015/2016 zinaonesha Mkoa wa Ruvuma ulilima Hekta 231,936.6 zilizotoa mavuno ya Tani 736,692.8 na katika msimu wa mwaka 2019/2020 Mkoa wa Ruvuma ulilima hekta 268,008 zilizotoa mavuno ya Tani 787,321 hii ni sawa na ongezeko la Tani 50,628.
Mndeme amesema Mafanikio hayo yametokana na uwepo wa nguvu kazi ya kutosha na utayari wa wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji ambapo hadi sasa Mkoa una chakula cha kutosha na ziada.
“Mkoa una jumla ya hekta 4,007,746 za ardhi zinazofaa kwa kilimo, katika kipindi cha Miaka mitano kuanzia mwaka 2015 - 2020 Mkoa umeweza kuzalisha tani 8,547,816 za mazao hadi kufikia mwaka 2020’’,alisisitiza.
Hata hivyo Mndeme ameyataja Mahitaji ya chakula katika Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka 2020 ni tani 469,172 ikilinganishwa na uzalishaji wa mazao ya chakula ni tani 1,346,220 na hivyo Mkoa una ziada ya chakula tani 877,048.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amemshukuru Rais wa Dkt John Magufuli kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ya kuboresha miundombinu ya barabara,,uwanja wa ndege wa Songea na miundombinu ya bandari katika ziwa Nyasa hali ambayo imeufanya Mkoa kupatikana barabarani,majini na angani.
Amesema miundombinu hiyo imetekelezwa na Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano na kwamba TANROADS ndiyo wadau wakuu katika utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba hivi sasa mtandao wa barabara kuunganisha Mkoa mzima wa Ruvuma unaendelea ambapo hivi sasa mradi wa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 67 kwa gharama ya shilingi bilioni 129 kutoka Mbinga kwenda Nyasa umefikia zaidi ya asilimia 52.
Kuhusu ujenzi na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Songea,Mndeme amesema hivi karibuni ndege aina ya bombadier zitaanza kutua katika uwanja huo ambao serikali imetoa shilingi bilioni 37 kukarabati na kuongeza urefu na kwamba mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya CHICCO ya nchini China upo katika hatua za mwisho hali ambayo itawezesha kurejesha tena safari za ndege ya bombadier mkoani Ruvuma,baada ya kusitishwa ili kupitisha ujenzi na ukarabati wa uwanja huo.
"Ruvuma ya sasa imefunguka sio sawa na Ruvuma ya zamani,nakupongeza sana Waziri wa Ujenzi,uchukuzi na mawasiliano kwa kusimamia miradi ya ujenzi ambayo inakwenda vizuri,serikali imetoa mabilioni ya fedha kukamilisha ujenzi wa barabara ya lami ya Mangaka mkoani Mtwara hadi Songea hali ambayo imeunganisha mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma kwa kuwa na mtandao wa lami'',alisema Mndeme.
Akizungumza kabla ya kufungua mkutano huo mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema Wizara yake imejitahidi kutekeleza miradi mbalimbali ambayo imechangia kuliingiza Taifa la Tanzania katika uchumi wa kati kutokana na ujenzi wa miundumbinu mbalimbali ya barabara,majini ya angani ikiwemo ununuzi wa ndege.
Mhandisi Kamwelwe amesema serikali ya awamu ya tano imejitahidi kutekeleza miradi mbalimbali kama ilivyo katika Ilani ya CCM ambapo mawasiliano kwa nchi nzima imefikia asilimia zaidi ya 90 na kwamba utekelezaji katika nishati ya umeme vimebakia vijiji 3000 tu kutekeleza katika nchi nzima na kwamba hivi sasa wananchi wanafurahi kuishi katika nchi yenye maendeleo makubwa na kwamba hivi sasa kuna dalili za vijiji kufutika kwa sababu kila kijiji kinaonekana ni mji mdogo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Agosti 4,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.