Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware akiambatana na ujumbe wake wamekutana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed
Zoezi hili ni mkakati endelevu wa ziara ya kuwatembelea Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ili kuhakikisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) inaendelea kuwafikia watanzania kwa kutoa elimu na kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya bima na hatimaye wawe watumiaji wazuri wa huduma na bidhaa za bima ili na wao wawe mabalozi kwa wengine.
Ruvuma ni mkoa wenye Wilaya tano zikiwemo Songea, Tunduru, Namtumbo, Mbinga na Nyasa na jumla ya Halmashauri nane. Huu ni moja ya mkoa Kusini mwa Tanzania wenye fursa nyingi za uwekezaji katika kilimo, uvuvi, ufugaji, uchumbaji wa madini na utalii. Kutokana na uwepo wa shughuli hizi za kiuchumi zinazochochea maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine ya jirani inayojumuisha Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni vema shughuli hizo, watu na mali zao wakapewa kinga ya bima.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) imetumia fursa hiyo kuzungumza na kutoa elimu ya bima kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuwawezesha na kuwajengea uelewa wa masuala mbalimbali yanayohusu bima ili nao waweze kuwa watumiaji wa bidhaa na huduma za bima na badae wawahamasishe Wanaruvuma.
Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware ameeleza kuwa Tira inatekeleza mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa (FYDP II-2020-2025) pamoja na Mpango Mkuu wa Taifa wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini (FSDMP-2020-2030) amabo unawataka watanzania wote kushiriki kwenye mpango huo kwa kuwa watumiaji na kuwa mabalozi kwa wengine.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameisisitiza sekta ya bima kuzingatia viwango vya utoaji wa huduma za bima kwa watanzania. Amesema kuwa muonekano wa miundombinu wa kutolewa huduma ikiwemo ofisi za watoa huduma za bima hususan kwa wakazi wa Ruvuma iboreshwe ili kuweka mazingira wezeshi na shawishi kwa wale wanaolengwa ili kuwahudumia kwa ueledi na ufanisi muda wote.
Dkt. Saqware amewahakikishia Wanaruvuma kuwa Mamlaka ipo na itaendelea kuwafikishia huduma za bima zenye tija na zenye manufaa huku soko la bima likibaki kuwa salama na linalosimamiwa kwa ueledi mkubwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.