MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas, amewataka wananchi kutunza mazingira kwa kuendelea kupanda miti katika maeneo yao ili kurudisha uoto wa asili utakaosaidia mkoa huo kuwa na uhakika wa kupata mvua mara kwa mara.
Laban Thomas, ametoa wito huo jana wakati akikabidhi miche ya miti ya matunda na mbao kwa viongozi wa kwaya ya mahakama kuu kanda ya Songea kwenye viwanja vya jengo la mahakama ya wilaya ya Namtumbo.
Alisema,ni muhimu kwa wananchi na taasisi za serikali mkoani Ruvuma,kuhakikisha wanaendelea na utamaduni wa kutunza mazingira kwa kuanzisha vitalu vya uoteshaji miche ya miti kama sera ya Taifa inavyosema.
Ameziagiza,serikali za vijiji,kata na wilaya kuhakikisha wanachukua hatua na kutumia sheria ndogo kudhibiti uharibifu wa mazingira katika maeneo yao ikiwamo kudhibiti uingiaji wa wafugaji na mifugo,badala ya kusubiri hadi pale hali inatakapokuwa mbaya.
Mkazi wa mtaa wa Minazini Namtumbo mjini Ali Ndauka,ameiomba serikali ngazi ya wilaya na mkoa kuchukua tahadhari ya kudhibiti uingizaji wa mifugo usiozingatia sheria kwenye baadhi ya vijiji wilayani humo.
Ndauka alisema,kama serikali haitachukua hatua madhubuti kukabiliana na vitendo hivyo basi kuna hatari kubwa ya wilaya ya Namtumbo na mkoa wa Ruvuma ambao bado una rasilimali kubwa ya ardhi na misuti kugeuka jangwa.
Alisema, baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji wamekuwa sehemu ya kuingia kwa wafugaji na mifugo yao wasiofuata taratibu kutokana na tamaa ya kupata fedha jambo linalo hatarisha wilaya ya Namtumbo kutokea kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa hapa nchini,inayotajwa kuwa na kasi kubwa ya uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji miti ovyo na uingizaji mifugo holela, hivyo kutishia mkoa huo unaotegemewa kwa uzalishaji wa chakula kugeuka jangwa kwa siku za baadaye.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.