Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa visima kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ambapo kwa awamu ya kwanza, halmashauri 4 za mkoa wa Ruvuma zitanufaika na mradi huo.
Akitoa taarifa katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika Kata ya Subira, Manispaa ya Songea, Mhandisi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Ruvuma, Lucia Chaula, amesema mradi huo wa uchimbaji visima vya umwagiliaji utaanza na halmashauri za Namtumbo, Madaba, Halmashauri ya Mbinga Vijijini, na Manispaa ya Songea.
Mhandisi Chaula ameeleza kuwa lengo la uchimbaji wa visima hivyo ni kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha wakulima wanaweza kuendelea kulima muda wote bila kutegemea mvua ambapo zaidi ya wakulima 540 watanufaika na visima hivyo, na zaidi ya ekari 760 zitatumia visima hivyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kanali Ahmed amesema fedha nyingi zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya mradi huo zinatarajiwa kuzaa matunda hivyo amesisitiza kuwa kazi hiyo inapaswa kufanyika kwa kasi, uaminifu, viwango na kwa ubora uliokusudiwa.
Amebainisha kuwa miradi hiyo ya uchimbaji wa visima ambayo itagharimu zaidi ya shilingi milioni 518 katika mikoa mitatu ya Njombe, Songwe, na Ruvuma ni uwekezaji endelevu wa Serikali katika kuhakikisha inapambana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya M/s MNFM Construction Co, S.L.P 634 Iringa, Mubarak Ngwada, amehaidi kufanya mradi huo kwa kiwango kinachostahili, hivyo wanahitaji ushirikiano wa wenyeji wa Kata ya Subira ambapo mradi huo utatekelezwa katika manispaa ya Songea ili waweze kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Mradi huo wa ujenzi wa visima vya umwagiliaji wenye thamani ya milioni 518,728,000 unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 6 (siku 180), na mkataba huo unajumuisha mikoa mitatu ya Songwe,Njombe na Ruvuma, ambapo kisima kimoja kitahudumia ekari 40 kwa wastani wa 2.5 kwa kila mkulima na kutimiza idadi ya wakulima 16 kwa kila kisima.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.