Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewahaidi wamachinga wa Manispaa ya Songea kuchangia mifuko 50 ya saruji na kugharamia uchimbaji shimo la choo chao.
Kanali Thomas ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza baada ya kusikiliza kero mbalimbali za wamachinga katika viunga vya Soko la Majengo Mjini Songea.
Amesema hapendi kuwaona wamachinga wanafanya biashara kwenye mazingira magumu ambapo amewataka wamachinga wote kufanya biashara kwenye maeneo waliyotengewa na serikali.
Kanali Thomas amewaomba wafanya biashara kuwa wazalendo katika kutoa pesa za kuchangia gharama za kuzolea taka Kwa mzabuni wao ili kuweka mazingira safi na salama ya Soko na mji wa Songea kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Kanali Thomas amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt Frederick Sagamiko kuwakamata watoto wa shule wanafanya biashara sokoni na Kwenda kuwaonesha wafanyabiashara wanaowatumikisha kufanya biashara badala ya Kwenda shule.
Katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa amemuuagiza Mwakilishi wa Meneja wa NMB Noela Minja kuendelea kutoa mikopo na elimu ya biashara kwa wamachinga ili wakuze biashara zao.
Minja amesema Benki ya NMB hadi sasa imetoa mikopo kwa wamachinga 35 ambao wamekidhi vigezo vya kupata mikopo,Meneja huyo pia ameahidi kutoa shilingi 100,000 kuchangia ujenzi wa choo cha wamachinga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt Frederick Sagamiko amehaidi katika ujenzi wa choo hicho kutoa bati na malipo ya fundi ili kukamilisha ujenzi kwa wakati.
Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa TANESCO Mashauri Adamu ameahidi kuchangia shilingi 300,000 kwa ajili ya ujenzi wa choo cha wamachinga.
Awali Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wadogo Mkoa wa Ruvuma Salum Masamaki amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufika kusikiliza kero za wamachinga na kuzitafutia ufumbuzi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.