Katika mkoa wa Ruvuma, ugonjwa wa malaria bado unaendelea kuwa changamoto kubwa ya kiafya, licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa kudhibiti maambukizi yake.
Kwa miaka mingi, malaria imekuwa chanzo kikuu cha wagonjwa hospitalini na hata vifo, hasa miongoni mwa watoto na kina mama wajawazito.
Kulingana na matokeo ya tafiti za Malaria zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kiwango cha maambukizi ya malaria mkoani Ruvuma kimeshuka kutoka asilimia 11.8 mwaka 2018 hadi asilimia 7.9 mwaka 2022.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr Louis Chomboko anasema Kushuka huku ni hatua muhimu, kwani kiwango hicho kiko chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 8.1 kwa mwaka 2022.
Maeneo Yenye Maambukizi Juu na Chini
Ingawa kiwango cha jumla kimepungua, baadhi ya halmashauri bado zina viwango vya juu vya maambukizi.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo inaongoza kwa asilimia 16, ikifuatiwa na Wilaya ya Tunduru yenye asilimia 15,vikiwa ni viwango maradufu ya wastani wa kitaifa.
Kwa upande mwingine, Halmashauri ya Mji wa Mbinga na Manispaa ya Songea zimeonesha mafanikio makubwa kwa kuwa na viwango vya chini vya maambukizi ya asilimia 5
Mikakati Madhubuti ya Kupambana na Malaria
Katika kutekeleza mpango wa kudumu wa kutokomeza malaria, Mkoa wa Ruvuma unaendesha kampeni chini ya kauli mbiu ya kitaifa: “Ziro Malaria Inaanza na Mimi”.
Mpango huu unalenga kuhusisha kila mwananchi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu kwa njia mbalimbali.
Mojawapo ya mikakati hiyo ni ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu kupitia programu ya School Net kwa wanafunzi mashuleni, pamoja na programu ya Chandarua Clinic kwa wajawazito na watoto wachanga kwenye vituo vya afya.
Hadi kufikia Desemba 2024, Mkoa wa Ruvuma ulikuwa umesambaza jumla ya vyandarua 363,378, ambapo 167,396 vilitolewa kupitia Chandarua Clinic na 195,982 kupitia School Net.
Udhibiti wa Mbu: Mazingira na Teknolojia
Mbali na ugawaji wa vyandarua, Mkoa pia umeimarisha mapambano kwa kutumia mbinu ya upuliziaji wa viuadudu kwenye mazalia ya mbu.
Mwaka 2024 pekee, jumla ya lita 1,200 za viuadudu zilitumika kupulizia mazalia ya mbu katika halmashauri mbalimbali.
Hatua Moja Baada ya Nyingine
Ingawa vita dhidi ya malaria bado haijamalizika, hatua zilizopigwa katika Mkoa wa Ruvuma zinaonesha kuwa mafanikio yanawezekana kupitia mshikamano wa jamii, usimamizi makini na mikakati ya kitaalamu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.