Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, wadau wa lishe pamoja na Taasisi binafsi, imefanya tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe na programu jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ngazi ya Mkoa kwa mwaka 2023/2024
Mgeni rasmi kwenye kikao cha tathmini hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea,Mheshimiwa Kapenjama Ndile.
Mkuu wa Mkoa ameitaja lishe bora kuwa ni silaha ya kupambana na maradhi, ambayo ni adui wa Taifa ndiyo maana tathmini ya lishe inafanyika kila robo ya mwaka kutokana na umuhimu wake
"Katika kupambana na adui maradhi, silaha mojawapo muhimu sana ni lishe. huwezi kupambana na maradhi katika Taifa kama lishe ya watu wako ni duni," amebainisha
Ameongeza kuwa suala la malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto linaenda sanjari na lishe, kwa kuwa kuboresha lishe kunapunguza uwezekano wa maradhi katika jamii na kuimarisha afya za watoto.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyasa,Mheshimiwa Peres Magiri, amesema kumekuwa na maendeleo mazuri kimkoa katika upande wa lishe na kwamba wilaya ya Nyasa inafanya juhudi kubwa kuhakikisha mkataba wa lishe unatekelezwa.
Ameitaja wilaya hiyo inafanya vizuri katika suala la lishe, ikinufaika na uwepo wa ziwa Nyasa linalowezesha upatikanaji wa samaki wanaotumika kutengeneza lishe
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto katika chakula kinachopelekwa mashuleni kwa ajili ya wanafunzi,ambacho kina ukosefu wa virutubisho ambapo ameahidi kulishughulikia suala hilo kwa kununua mashine ambazo zitaongeza thamani katika uandaaji wa lishe
Mpango jumuishi wa masuala ya lishe nchini unatoa muongozo wa utekelezaji wa afua za lishe, ukilenga kuimarisha mikakati ya kukabiliana na aina zote za utapiamlo kwa watu wa rika mbalimbali.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.