Viongozi wa dini, serikali na waumini wa madhehebu mbalimbali mkoani Ruvuma wameungana katika ibada maalum ya maombi ya siku saba, wakiombea amani, umoja na mshikamano wa Tanzania, hususan wakati huu wa mabadiliko makubwa ya kijamii na kisiasa.
Akihudhuria ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Pentecostal Hema ya Makutano, kijiji cha Namtuhi, Halmashauri ya wilaya ya Songea, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abass Ahmed, aliwakilishwa na Afisa Utamaduni wa Mkoa, Anthony Luoga,alisisitiza wajibu wa kila raia kulinda amani ya taifa, akibainisha kuwa amani ni tunu adimu, inayopotea kwa urahisi lakini ni ghali sana kuirudisha.
“Kulinda amani ya taifa letu ni jukumu la kila mmoja. Amani ni tunu tuliyopewa, lakini si rahisi kuipata tena pindi inapotoweka. Tushirikiane sote kuilinda, tuishabikie, na tuirithishe kwa vizazi vijavyo,” alisema Luoga, akihamasisha umma kudumisha umoja, upendo na mshikamano.
Aliwataka wazazi na walezi kuzingatia malezi bora, hususan ya kidini, ili kuzuia wimbi la vijana wanaotumia mitandao ya kijamii kutoa maneno ya matusi, kejeli, na dharau, hususan dhidi ya viongozi wa dini, kisiasa na jamii. Alisisitiza kuwa, malezi mazuri yanaleta raia wema, wanaoheshimu madaraka, taratibu na utawala wa sheria.
Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu wa Kanisa la Pentecostal Hema ya Makutano, Javery Eliakimu, alisema ibada hiyo ni sehemu ya siku saba za maombi ya kuliombea taifa, viongozi wa serikali, na jamii kwa ujumla. Alibainisha kuwa lengo ni kuwaombea viongozi wafanye uamuzi wa busara, wa haki, na wa maendeleo, huku wakiimarisha umoja wa kitaifa.
“Jukumu letu kama viongozi wa dini si kuhukumu, wala kuchochea chuki, bali ni kuliombea taifa na viongozi wake. Tukiungana, tutaijenga Tanzania imara, yenye amani, umoja na maendeleo ya kweli,” alisema Askofu Eliakimu, akihimiza waumini kuendelea kuliombea taifa, viongozi wake na jamii.
Maombi hayo yameshirikisha waumini, viongozi wa dini, wazee wa kanisa, viongozi wa serikali ya mkoa, na wananchi wa kawaida, ambao walijitokeza kwa wingi, kuonyesha mshikamano wa kidini, umoja na upendo wa taifa. Ikumbukwe, Kanisa la Pentecostal Hema ya Makutano limeandaa mfululizo wa ibada kama hizi, zinazolenga kuimarisha amani, umoja, na maendeleo ya Tanzania.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.