Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya ujenzi wa kampasi ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) katika Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa IAA Kampasi ya Songea, Dkt. Bakari Mashaka alisema kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Rais Samia kuhakikisha kila mkoa unakuwa na chuo kikuu ili kuboresha elimu ya juu nchini.
Kwa mujibu wa Dkt. Mashaka, chuo hicho kipya kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 10,000 na kitaanza kujengwa mara moja kwa kutumia mfumo wa ‘force account’. Alisema kwa sasa IAA Kampasi ya Songea inatoa kozi mbalimbali zikiwemo za diploma na shahada katika nyanja za biashara, uhasibu, fedha, benki, TEHAMA na uongozi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Dkt. Mwaitete Cairo, alieleza kuwa Manispaa ya Songea imetoa eneo lenye ukubwa wa hekari 71 katika Kata ya Tanga kwa ajili ya ujenzi huo. Alibainisha kuwa mradi huo utatoa ajira kwa wakazi wa Songea pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi kutokana na uwepo wake karibu na miundombinu kama stendi kuu ya mabasi, machinjio ya kisasa na hospitali ya rufaa.
Afisa Uhusiano wa IAA Kampasi ya Songea, Nuru Meshack, aliwahamasisha vijana kuchangamkia fursa za elimu akibainisha kuwa hata wanafunzi waliopata daraja la nne wanaweza kujiunga na masomo ya diploma, kinyume na imani ya baadhi ya wazazi.
Meya wa Manispaa ya Songea, Michael Mbano, alilipongeza chuo hicho kwa hatua hiyo na kusema kuwa limejibu kilio cha muda mrefu cha wananchi kutaka taasisi za elimu ya juu mkoani humo.
Wakati huo huo, IAA imejipanga kuanzisha madarasa ya mtandaoni ili kutoa elimu kwa wanafunzi walioko katika kampasi zake za Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Babati, Songea na hata nje ya nchi ikiwemo Sudan Kusini na Comoro, hatua itakayowezesha mafunzo kutolewa kwa wakati mmoja kimataifa
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.