SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje imedhamiria kuyarejesha nchini mafuvu 200 ya mashujaa yaliyohifadhiwa nchini Ujerumani.
Mafuvu hayo likiwemo fuvu la Jemedari wa kabila la wangoni Nduna Songea Mbano yalichukuliwa na wajerumani mwaka 1906 kutokana na mashujaa hao kuonesha upinzani mkubwa dhidi ya utawala wa wakoloni katika vita ya Majimaji iliyopiganwa kati ya mwaka 1905 hadi 1907.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Aloyce Nzuki anasema mafuvu hayo yakirejeshwa nchini ,yatafanyiwa maziko ya heshima yanayostahili kwa mashujaa.
Anasema kwa miaka mingi kumekuwa na mjadala unaohusu urithi wa nchi yetu uliochukuliwa na kuhifadhiwa nje ya nchi yakiwemo mafuvu ya mashujaa wa vita ya Majimaji yaliopo Ujerumani kurejeshwa nchini.
Hata hivyo anasema,Wizara imebaini baadhi ya mafuvu ya mashujaa hao yalitoka Songea na kwamba Wizara inaahidi kushirikiana na jamii zote za kitanzania zenye kudai urithi huo kurejeshwa nchini kwa kuainisha aina za urithi unaopaswa kurejeshwa nchini.
“Madai ya urithi huo yatawasilishwa rasmi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje,ndugu zetu wangoni,tunahitaji kurejesha heshima kwao kwa sababu wao walitupa heshima kubwa ya kulinda,nchi yetu,mila na desturi zetu’’,anasema Dkt Nzuki.
Anaitaja aina moja muhimu ya kurejesha heshima kwa wangoni ni kurejesha mafuvu ya mashujaa hao ili yaweze kupatiwa maziko ya heshima na kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii ipo tayari kuhakikisha mafuvu hayo yanarejea nchini.
Akizungumzia umuhimu wa kuwakumbuka mashujaa katika harakati za ukombozi,Dkt.Nzuki anasisitiza watanzania kutambua na kujifunza utamaduni wa jamii ya wangoni hasa namna mababu zetu walivyojitoa muhanga kupinga uonevu wa kikoloni wa kijerumani na kuamua kupigana nao.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Septemba 23,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.