Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kumekuwa na malalamiko katika mfumo wa utoaji haki, ucheleweshwaji wa kesi, kutoridhishwa na maamuzi na malalamiko ya rushwa katika mahakama.
Amesema katika muundo wa Mahakama kuna Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo kazi yake ni kupokea malalamiko ya watumishi wa Mahakama pale ambapo wananchi wanaona hawajatendewa haki .
Amebainisha kuwa katika ngazi ya Mkoa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Mahakama ni Mkuu wa Mkoa na Wilaya ni Mkuu wa Wilaya, ambapo wananchi wanapaswa kutambua uwepo wa kamati hizo na kuwasilisha malalamiko yao pale wanapoona hawajatendewa haki ili yafanyiwe kazi.
Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameasisi kampeni ya Mama Samia Legal Aid ambayo tayari ipo katika mikoa 22 nchini kuwahudumia wananchi wenye uhitaji, amesema kampeni hiyo inalenga kutoa Elimu ya Sheria kwa wananchi na utatuzi wa migogoro.
Mhe. Ndumbaro amesema Mheshimiwa Rais ameruhusu ajira za maafisa maendeleo ya jamii katika kila Halmashauri ambao wapo katika maeneo ya kazi na wanaendeleza huduma ya msaada wa kisheria, kusikiliza kero za wananchi na kuzipeleka kwa wataalam wa kisheria waliopo kwenye maeneo husika na kuifanya kampeni ya Mama Samia Legal Aid kuwa endelevu.
Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais kupitia muhimili wa Mahakama ameamua kuwajengea wananchi wa mkoa wa Ruvuma kituo jumuishi cha Mahakama katika kata ya Msamala Manispaa ya Songea, ambacho kitajumuisha Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani hivyo kuwaondolea wananchi adha ya kusafiri hadi Iringa kuifuata Mahakama ya Rufani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.