WIZARA ya Kilimo katika mwaka huu wa fedha imetenga shilingi bilioni 384 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji huku kiasi kikubwa cha fedha kinatarajia kupelekwa mkoani Ruvuma kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha umwagiliaji.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Antony Mavunde wakati anazungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Mbambabay na Liuli wilayani Nyasa ambapo amesema serikali inapeleka fedha katika Bonde la Mto Ruhuhu wilayani Nyasa lenye ukubwa wa hekta 3700 ili kuanzisha kilimo cha umwagiliaji.
“Mwishoni mwa mwezi huu tutamtangaza Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kufanya upembezi yakinifu na usanifu wa kina Pamoja na ujenzi wa Bonde lote la Mto Ruhuhu ambalo litawaruhusu wakulima kuendesha kilimo cha umwagiliaji’’,alisema.
Hata hivyo amesema katika bajeti ya mwaka huu,Wizara ya Kilimo imepanga kujenga mabwawa 100 katika nchi nzima na kwamba bwawa moja litajengwa katika wilaya ya Nyasa Kijiji cha Lundo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Naibu Waziri huyo amebainisha zaidi kuwa serikali katika mwaka huu wa fedha imetenga fedha kwa ajili ya kujenga skimu tatu za umwagiliaji wilayani Nyasa ambapo amezitaja skimu hizo kuwa ni skimu ya Chiulu yenye ukubwa wa hekta 7000,Lundo hekta 600 na skimu ya Kimpange hekta 400.
Amesisitiza kuwa serikali imedhamiria kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa Mkoa wa Ruvuma ni ghala la taifa la chakula na Mkoa unategemewa na nchi katika uzalishaji wa mazao ya chakula.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Thomas amesema Mkoa wa Ruvuma una utoshelevu wa chakula na kuwa na ziada na kwamba Chakula kilichozalishwa katika msimu 2022/2023 kinatarajia kutumika hadi msimu wa 2023/2024 ambapo mazao ya chakula zilizalishwa tani 1,598,163 na kati ya hizo zao la mahindi zimezalishwa jumla ya tani 1,043,324.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.