SERIKALI ya Awamu ya Tano imetoa jumla ya shilingi milioni 500 kuboresha kituo cha afya Muhukuru kilichopo wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa uboreshaji wa kituo hicho Mganga Mfawidhi wa kituo Dr.Denis Mhagama amesema fedha hizo zilipokelewa katika mwaka wa serikali 2017/2018 na kwamba kazi ya ujenzi ilikamilika Machi mwaka huu.
Ameyataja majengo ambayo yamekamilika kuwa ni jengo la upasuaji,maabara,jengo la kuhifadhia maiti,nyumba ya mtumishi na wodi ya mama na mtoto.
Dr.Mhagama amezitaja huduma zinazotolewa katika kituo hicho kuwa ni matibabu ya wagonjwa wa nje,matatibu ya wagonjwa wa ndani,huduma ya mama na mtoto,upimaji wa VVU na ushauri nasaha.
Amezitaja huduma nyingine kuwa ni kliniki ya watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI,uchunguzi wa viashiria vya saratani ya shingo ya kizazi kwa akinamama,matibabu ya kifua kikuu na ukoma na huduma za upasuaji hasa kwa akinamama wenye uzazi pingamizi.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Watu wenye ulemavu Jenista Mhagama ameishukuru serikali na Ubalozi wa Japan kwa kutoa fedha za kuboresha kituo cha afya Muhukuru.
Amesema kituo hicho kinahudumia kata tatu za Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambazo ni Lilahi,Muhukuru na Ndongosi na kwamba kituo hicho pia kinatoa huduma kwa baadhi ya maeneo ya wilaya ya Nyasa na nchi jirani ya Msumbiji.
“Kukamilika kwa majengo haya kumewezesha kuokoa kwa kiasi kikubwa vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga,ambavyo vingeweza kutokea kutokana na umbali wa kituo na hospitali ya Mkoa’’,alisema.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Simon Bulenganija amesema katika uboreshaji wa kituo hicho Halmashauri imechangia sh.milioni 28.2 na kwamba upatikanaji wa dawa na vitendanishi katika kituo ni zaidi ya asilimia 90 kwa walengwa wapatao 20,620.
Kituo cha Afya Muhukuru kipo umbali wa kilometa 80 kutoka makao makuu ya Halmashauri ya Songea,kikiwa na watumishi 25 wa kada mbalimbali.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 10,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.