SERIKALI YATOA MILIONI 500 HALMASHAURI YA MADABA KUJENGA LAMI KM MOJA
SERIKALI ya awamu ya Tano imetoa jumla ya sh.milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya lami nyepesi ya kilometa moja katika Halmashauri ya Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Meneja wa TARURA Halmashauri ya Madaba Mhandisi Razaro Kitomari amesema fedha hizo zinajenga barabara ya Kipingo-Lita na kwamba mkataba wa mradi huo ni wa siku 180 ambao umeanzia Aprili 7 mwaka huu na unatarajia kumalizika Oktoba 6 mwaka huu.
Amesema utekelezaji wa mradi huo hadi sasa ni Zaidi ya asilimia 50 na kwamba lengo la TARURA ni kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa barabara hiyo kabla ya mkataba ambapo amesema hadi sasa kazi inakwenda vizuri kwa kuwa vifaa vyote vinavyohitajika vipo katika eneo la mradi.
“Katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 Halmashauri ya Madaba ni miongoni mwa Halmashauri 65 nchini ambazo zimepatiwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi za viongozi katika program ya ,maendeleo’’,alisema Kitomari.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo,Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Ruvuma Odo Mwisho ameipongeza Halmashauri ya Madaba kwa kushirikiana na TARURA kwa kutekeleza mradi huo ambao unakwenda kuondoa changamoto ya ubovu wa barabara hiyo.
Ametoa rai kwa TARURA kuhakikisha kuwa wanajenga barabara hiyo katika viwango ambavyo vitaiwezesha barabara kudumu kwa muda mrefu kwa kuwa serikali inatoa fedha za walipa kodi ambazo zinatakiwa kutumika kulingana na thamani ya mradi uliotekelezwa.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 13,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.