SERIKALI YATOA SHILINGI BILIONI 3.12 KUANZA UJENZI WA MADARASA 156 RUVUMA
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 3.12 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 156 mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea katika kikao kazi cha maelekezo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari 2023.
Akizungumza kwenye kikao hicho kilichowashirikisha watendaji ngazi ya Mkoa na wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma,Kanali Thomas amempongeza Rais kwa jitihada zake za kuhakikisha anaondoa tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari.
“kwa mara nyingine tena Mkoa wetu umepokea shilingi bilioni 3.12 kutoka kwa Mhe.Rais kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 156 katika shule za sekondari,ujenzi unatakiwa kukamilika Desemba 15,2022 ambayo ni sawa na siku 75 tu hivyo hatuna budi kufanya kazi usiku na mchana’’,alisisitiza Kanali Thomas.
Ili kuhakikisha majengo hayo yanakamilika kwa wakati,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameagiza wilaya zote kuimarisha dhana ya ushirikishwaji na uwajibikaji,Halmashauri zote kuunda kamati za usimamizi wa miradi na kuanza mchakato wa manunuzi ya vifaa na upatikanaji wa mafundi wenye uwezo.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameagiza usimamizi na ufuatiliaji wa ngazi zote ufanyike ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kwa ubora.
Akizungumza kwenye kikao hicho Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki amesema Mkoa wa Ruvuma kupitia Mamlaka ya Serikali za Mitaa TAMISEMI umepokea kiasi cha shilingi bilioni 3.12 kutoka serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 156 katika shule za sekondari 68.
Ameyataja maelezo mahususi ya utekelezaji wa mradi huo kuwa ni kufuata mwongozo wa force account katika utekelezaji wa mradi na kutumia ramani ya darasa iliyoelekezwa kwenye program EP4R na UVIKO 19.
Maelekezo mengine ameyataja kuwa ni kuhakikisha ujenzi unakamilika ifikapo Desemba 15,2022 na utekelezaji wa miradi yote uzingatie thamani ya fedha na ubora wa miradi.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Ruvuma anayeshughulikia Mipango Jumanne Mwankoo amebainisha kuwa kati ya shilingi bilioni 3.12 zilizotolewa,Manispaa ya Songea imepokea shilingi bilioni 1.52 kwa ajili ya kujenga vyumba 76 vya madarasa.
Mwankoo ameitaja Halmashauri ya Mbinga Mji kuwa imepokea shilingi milioni 220 kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa 11,Halmashauri ya Namtumbo imepokea shilingi milioni 340 kwa ajili ya kujenga madarasa 17 na Halmashauri ya Nyasa imepokea sh. Milioni 240 kwa ajili ya kujenga madarasa 12.
Kulingana na Katibu Tawala huyo,Halmashauri ya Songea ,Halmashauri ya Mbinga, na Halmashauri ya Madaba kila mmoja imepokea shilingi milioni 200 kwa ajili ya kujenga vyumba kumi vya madarasa.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Ndugu Odo Mwisho amewashauri watendaji kuhakikisha wanajenga madarasa hayo katika ufanisi na viwango vinavyolingana na fedha zilizotolewa na serikali na kwamba mapungufu yaliyojitokeza kwenye madarasa ya UVIKO yasijirudie tena.
Katika Mwaka wa fedha 2021/2022,Mkoa wa Ruvuma ulipokea sh.bilioni 10 kupitia fedha za UVIKO zilizowezesha kujenga vyumba vya madarasa 500 katika shule za msingi na sekondari.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
Oktoba 4,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.