Katika kijiji kidogo cha Mitomoni kata ya Mipotopoto, pembezoni mwa Pori la Akiba la Liparamba wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, simulizi ya nadra na ya kusikitisha imetokea simba mnweye rangi ya kahawia na nyeupe, kiumbe adimu anayepatikana katika maeneo machache sana duniani, ameuawa baada ya kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha taharuki kubwa.
Kwa muda mrefu, wakazi wa kijiji hicho wameishi kwa amani, wakifahamu kuwa hifadhi ya Liparamba ni jirani yao, lakini si hatari kwao. Lakini siku nne zilizopita, hali hiyo ilibadilika ghafla.
Diwani wa Kata ya Mipotopoto Mheshimiwa Said Mahamud, anasimulia tukio la mwananchi mmoja aliyenusurika kifo baada ya kukutana uso kwa uso na simba huyo porini.
“Alikuwa njiani kutoka shambani, alipokutana na simba huyo. Aliweza kujiokoa kwa kupanda mti na kutumia matawi kujilinda, kabla ya simba huyo kuondoka,” anasema Mahamud.
Lakini kama tukio hilo halikutosha kuibua hofu, usiku wa kuamkia Aprili 15, simba huyo alifanya kile kinachoonekana kama shambulizi la kipekee, alipanda paa la nyumba, akashika mbwa, kubomoa dirisha, na hata kuchukua nguo kabla ya kutoweka gizani.
Kulingana na Diwani huyo Usiku uliofuata, simba huyo akaingia zizini na kuua kondoo watano na mbuzi mmoja wa mwananchi Said Njete.
Kilichofuata ni hatua ya haraka ya Serikali kupitia askari wa wanyamapori wa Pori la Akiba Liparamba waliowasili kutoka Mbinga.Baada ya ufuatiliaji, waliweza kumuua simba huyo na kuchukua ngozi yake.
Kwa mujibu wa diwani huyo, simba huyo alikuwa ni dume mwenye rangi ya kahawia na nyeupe ,maelezo yanayowiana na tabia ya simba adimu duniani wanaopatikana tu katika Pori la Akiba la Liparamba.
Inasemekana kuwa simba huyo alikuwa dhaifu na mwenye dalili za ugonjwa, jambo ambalo huenda lilimfanya kuvuka mipaka ya pori na kuingia kwenye makazi ya binadamu.
“Kwa miaka mingi hatujawahi kushuhudia simba wakiingia hadi nyumbani kwa watu. Hili ni tukio la kwanza la aina yake,” alisema Mheshimiwa Mahamud.
Wananchi wa Mipotopoto wameipongeza Serikali kwa hatua ya haraka iliyochukuliwa, wakisema kuwa simba huyo angeweza kuleta maafa makubwa iwapo asingedhibitiwa.
Askari wa wanyamapori wamewataka wananchi kutoa taarifa mapema kila wanapoona wanyama hatari ili kuzuia majanga makubwa.
Pori la Liparamba, ambalo linapakana na nchi ya Msumbiji, ni moja ya hazina za kipekee za taifa, likiwa na mandhari ya kuvutia na wanyama adimu kama tembo na simba weupe wa ajabu, pori hili linatajwa kuwa na uwezo wa kugeuka kuwa moja ya vivutio vikuu vya utalii wa kipekee barani Afrika.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.