MJI wa Songea uliopo katika Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa maeneo machache hapa nchini ambayo yana hazina kubwa ya utajiri wa kihistoria na kishujaa.
Mashujaa kutoka katika Mji wa Songea waliendeleza mapambano dhidi ya ukoloni wa Kijerumani hivyo kuchangia kikamilifu harakati za ukombozi kabla ya kupata uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.
Jina la Mji wa Songea ni kumbukumbu ya Nduna Songea Mbano ambaye alikuwa na Ikulu yake katika Mji wa Songea.Mji wa Songea una majengo ya kumbukumbu za kihistoria mbalimbali yakiwemo makanisa yenye miaka zaidi ya 100.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Bartazar Nyamusya anasema historia inaonesha kuwa Mji wa Songea ulianzishwa mwaka 1897 kama kituo cha kijeshi cha Kijerumani.
“Mji wa Songea uliendelea kukua na kuwa Makao makuu ya utawala wa Wajerumani katika Wilaya ya Songea,Mji huo ulizinduliwa rasmi kuwa mji wa kihistoria,kishujaa na kiutalii mwaka 2010’’,anasema Nyamusya.
Hata hivyo Nyamusya anabainisha kuwa Mji wa Songea uliathirika na Vita ya Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907 na Vita kuu ya pili ya Dunia kati ya mwaka 1939 hadi 1945.
Licha ya Mji huo kuathirika na vita hivyo,uliendelea kuwa Makao makuu ya Mkoa wa Ruvuma wakati wa utawala wa Waingereza katika Tanganyika,baada ya uhuru hadi leo bado Songea ndiyo Makao Makuu ya Mkoa wa Ruvuma.
Anasema Mji wa Songea una umaarufu wa mashujaa wa Vita vya Majimaji ambapo mashujaa 67 walinyongwa mwaka 1906 kati yao mashujaa 66 walizikwa katika kaburi moja.
Nyamusya anabainisha kuwa Nduna Songea Mbano ambaye alikuwa na umaarufu,alinyongwa na kuzikwa katika kaburi lake ambapo makaburi yote yapo katika Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.
Mashujaa hao 67 walinyongwa katika eneo lililojengwa Mnara wa Mashujaa wa vita vya Majimaji nyuma ya ukumbi wa Songea ambalo ni kivutio cha aina yake cha utalii katika Mji wa Songea .
Mhifadhi huyo wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji anasema Mkoa wa Ruvuma pia ulitoa mashujaa walioshiriki katika Vita kuu ya pili ya Dunia ambapo mashujaa 270 walishiriki katika vita hiyo kati yao mashujaa watatu walikuwa ni wanawake.
Akizungumzia kuhusu Makumbusho ya Majimaji,Nyamusya anasema yalianzishwa rasmi mwaka 1980 na kusimamiwa na Hayati Dk.Lawrence Gama wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Hata hivyo anasema mchakato wa kuyakabidhi Makumbusho hayo chini ya Shirika la Makumbusho ya Taifa ulianza Mei hadi Novemba 2009 ukisimamiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma.
Makumbusho hayo yalikabidhiwa katika Shirika la Makumbusho ya Taifa chini ya sheria ya makumbusho ya Taifa la Tanzania,namba saba ya mwaka 1980 hivyo makumbusho hayo yalipandishwa hadhi na kuwa Makumbusho ya Taifa mwaka 2010.
“Haya ni Makumbusho pekee nchini ambayo imebahatika kuwa na vifaa muhimu katika historia ya Mtanzania ,mchakato uliopo hivi sasa ni Makumbusho hayo kuchukuliwa kuwa ya Kitaifa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili iwe endelevu”,anasisitiza Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa.
Anabainisha zaidi kuwa Mji wa Songea ni miongoni mwa miji michache ambayo ilitoa upinzani mkali katika vita vya Majimaji ambapo katika Makumbusho hayo kuna ushahidi ambao unaonesha moja kwa moja kuwa wazee wa Songea walishiriki kikamilifu katika vita hivyo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.