Halmashauri ya wilaya ya songea mkoani Ruvuma imefanikiwa kutoa mshindi wa kwanza kimkoa na mshindi wa pili katika Kanda ya Nyanda za Juu katika ufugaji wa samaki.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa mshindi na Naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Aksoni katika maonesho ya nane nane yaliyo fanyika katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya hivi karibuni.
Afisa Mifugo wa Halmashauri ya wilaya ya songea Dkt Erick Kahise amemtaja aliyeshinda tuzo hiyo kuwa ni Aureliusi Njerekela kutoka kijiji cha Peramiho nje kidogo ya mji wa Songea.
Dkt Kahise amesema mfugaji huyo ameshinda tuzo hiyo baada ya kushindanishwa na wafugaji ndani ya Mkoa na Mikoa ya Nyanda za juu kusini na kuibuka kinara katika ufugaji wa samaki.
”Ufugaji wa samaki ni fursa inanyomwinuia kiuchumi mwananchi hivyo wananchi wanatakiwa kufanya ufugaji wa samaki ili kujikwamua kiuchumi”,alisema Dkt Kahise.
Kwa upande wake Bw Njelekela amesema yeye binafsi ana mapenzi makubwa ya ufugaji wa samaki na alianza kufuga samaki mwaka 2016 na amendelea kufuga hadi sasa akiwa na mabwawa sita.
Amesema kupitia elimu ya ufugaji ambayo ameipata kutoka kwa wataalamu imemsaidia kuendelea kufuga kwa kisasa kwa kutumia mabwawa ya maturubai njia ambayo inatoa mazao mazuri ya samaki ukilinganisha na mabwawa ya matope ambayo wakati wa kuvua,samaki hukimbilia kwenye mapango hivyo husababisha hasara kwa wafugaji.
Dr.Kahise amesema Halmashauri ya Wilaya ya Songea haina changamoto za magonjwa ukilinganisha na mikoa mingine na kwamba maeneo mengi yana maji ya kutosha katika kipindi kizima cha mwaka hivyo kusababisha ufugaji wa samaki kuwa ni fursa kwa mtu yeyote anayependa kufuga.
Ametoa wito kwa wafugaji wa samaki kuanza kufuga kwa kuchimba mabwawa nchi kavu ,mabwawa ambayo hayana karaha katika utunzaji wa samaki.
Ametoa rai kwa wafugaji kuanza kufuga kambale ambao wanaoneka kuwa na bei ya wastani wa shilingi ya 8000 kwa kilo moja ambapo kambale mmoja anaweza kuwa na zaidi ya kilo tatu ukilinganisha na pelage wenye kilo ndogo.
Halmashauri ya wilaya ya songea inatarajia kuanzisha kituo cha uzalishaji wa vifaranga vya samaki katika eneo la Lundusi ambapo kila mwananchi atapata fursa ya kujifunza na kununua vifaranga vya samaki.
Imeandikwa na
Jacquelen Clavery
Afisa habari –Songea DC.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.