Na Albano Midelo
MIONGONI mwa madhara makubwa ya rushwa kwenye uchaguzi yametajwa kuwa ni kunyima haki ya kuchagua kiongozi bora na anayehitajika hivyo kukwamisha maendeleo kutokana na viongozi waliopatikana kwa njia ya rushwa.
Hayo yamesemwa na Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Yahaya Mwinyi wakati anatoa mada ya nafasi ya wanahabari katika mapambano ya rushwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 2024 na uchaguzi Mkuu 2025.
TAKUKURU wameandaa mafunzo hayo kwa wanahabari 21 kutoka vyombo mbalimbali vya Habari wilayani Songea ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa TAKUKURU Mahenge Manispaa ya Songea.
Mwinyi ameyataja madhara mengine ya rushwa kwenye uchaguzi kuwa ni wananchi wanadharirika kwa kuthaminishwa na vitu vidogo kama pombe na zawadi ili kuwachagua viongozi wasiokuwa na sifa hivyo jamii kukosa huduma muhimu kama zahanati,umeme na maji.
“Madhara ya rushwa kwenye uchaguzi,wananchi kupata viongozi wasiokuwa waadilifu na kuongezeka kwa umasikini kwa sababu viongozi waliochaguliwa wanakosa sifa za kuwaletea maendeleo wananchi’’.alisisitiza Mwinyi.
Awali akizungumza kwenye ufunguzi na ufungaji wa mafunzo hayo Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Janeth Haule amesema TAKUKURU imeamua kufanya mafunzo hayo kwa wanahabari kwa kutambua Taifa linaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Amesema wanahabari wana mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa kwa sababu wanahabari ni kioo cha jamii na wana uwezo mkubwa wa kuwafikia wananchi wengi kwa haraka.
“Vyombo vya Habari vinaaminika sana kwa wananchi kwa hiyo tumeona tuanze kutoa mafunzo haya kwanza kwa wanahabari na baadaye tutaingia katika makundi mengine’’,alisema Haule.
Amesisitiza kuwa vyombo vya Habari vina nafasi kubwa ya kuzuia rushwa kwenye uchaguzi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
Ameutaja wajibu wa vyombo vya Habari hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa ni kubadili fikra za wananchi kulingana na misingi ya maadili,uadilifu,utawala bora,haki za binadamu,uzalendo na upendo.
Amesema rushwa inakatazwa kila mahali ambapo kisheria rushwa ni kosa la jinai,rushwa pia ni utovu wa maadili kwa jamii na dini zote zimetamka wazi kuwa rushwa ni dhambi.
TAKUKURU Ruvuma itaendelea na uelimishaji wa madhara ya rushwa kwenye uchaguzi kwa kutoa elimu katika makundi mbalimbali yakiwemo wanahabari,viongozi wa dini,viongozi wa vyama vya siasa na kuendelea kuwaelimisha wananchi kwa ujumla kuhusu mapambano dhidi ya rushwa kuelekea kwenye uchaguzi
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.