Na Gustaph Swai-RS Ruvuma
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Chuo cha Utumishi wa Umma, imetoa mafunzo maalum kwa Maafisa Tarafa na Maafisa Watendaji wa Kata katika Mkoa wa Ruvuma
Mafunzo hayo yanatolewa kwa siku mbili katika Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, yakilenga kuwawezesha viongozi hao kuboresha utendaji kazi wao wa kila siku kwa kuzingatia sheria, taratibu, na miongozo ya serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo amewataka maafisa tarafa na watendaji kata kushughulikia kero za wananchi kwa haraka akiwasisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa kutatua matatizo yanayowakabili wananchi katika maeneo yao.
"Nilazima tujenge Hali ya umiliki kwa kazi tulizopewa, na baada ya kujenga hiyo hali ya umiliki ni lazima tusikilize na kutatua kero za wananchi ili watuone sisi ni msaada kwao na watukimbilie’’,alisisitiza.
Ameongeza kuwa uzoefu unaonesha kuwa zimekuwepo changamoto nyingi ambazo zinaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi katika ngazi ya kata na tarafa zinazotokana na kutokuzingatiwa kwa kanuni, sheria na taratibu katika utendaji kazi.
Mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Afisa Tarafa wa Peramiho Salma Mapunda, amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo na kuwakumbusha utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo usimamizi wa miradi na usimamizi wa ununuzi ndani ya tarafa.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawaongezea uwajibikaji ili kuleta maendeleo na kutatua kero za wananchi kwa kusimamia utawala bora wenye uwazi na Uwajibikaji
Ofisi ya Rais TAMISEMI hadi sasa tayari imeshatoa mafunzo hayo kwa mikoa 20 kati ya 26 ya Tanzania Bara.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.