Mkuu wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma Mheshimiwa Peres Magiri ameipongeza Tarafa ya Mpepo wilayani humo kwa kufanikiwa kutoa chakula cha mchana kwa shule zake zote.
Ametoa pongezi hizo wakati anazungumza kwenye kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa katika kipindi cha kuanzia Aprili hadi Juni 2024 ambacho kimefanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kilosa Mbambabay.
Amewaagiza watendaji wote wa Kata na wadau wa afya na lishe kusimamia utekelezaji wa shule zote kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi ili kupunguza udumavu unaoikabili Wilaya ya Nyasa na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
“Nawaagiza watendaji Kata wote katika wilaya ya Nyasa,kuhakikisha shule zote zinatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi kwa sababu haya ni maamuzi yaliyopitishwa kwenye vikao vya vijiji na Kata’’,alisisitiza.
Sanjari na agizo hilo,Mkuu wa Wilaya pia ameagiza kila shule angalau iwe na bustani ya mboga ili kupata lishe bora kwa sababu,shule zinazotoa chakula cha mchana kwa wanafunzi sehemu kubwa , wanafunzi wanakula kande za mahindi yaliyokobolewa hivyo kukosa virutubisho muhimu na kusababisha udumavu kuendelea.
Taarifa ya tathmini ya Mkataba wa lishe katika Halmashauri ya Nyasa iliyotolewa katika kikao hicho,inaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Aprili hadi Juni 2024 jumla ya wanafunzi 49,161 kati ya 58,191 wanapata angalau mlo mmoja wawapo shuleni sawa na asilimia 84.48 .
Kulingana na taarifa hiyo katika kampeni iliyofanyika Mwezi Juni mwaka huu, Watoto 23,504 kati ya 23,504 sawa na asilimia 100 walipatiwa matone ya vitamini A.
Hata hivyo taarifa hiyo inaonesha kuwa katika kipindi hicho Watoto 15 kati ya 14,665 sawa na asilimia 0,001 waligundulika na utapiamlo mkali na kwamba wote walipatiwa matibabu.
Ili kukabiliana na utapiamlo na udumavu wilayani Nyasa,baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa kwenye kikao hicho ni Pamoja na shule zote za msingi na sekondari kulima bustani za mboga,matunda na kuendelea kuhamasisha wanafunzi shuleni kutumia unga ulioongezwa virutubisho.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.