SERIKALI kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA imetumia kiasi cha Sh.milioni 629 kujenga daraja jipya katika mto Nanjoka linalounganisha kata ya Nakayaya na Majengo wilayani Tunduru.
Ujenzi wa daraja hilo,unatokana na daraja la zamani kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa zilizonyesha mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu ambazo zilileta maafa makubwa kwa wananchi na kuharibu miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Meneja wa TARURA wilayani Tunduru Mhandisi Silvanus Ngonyani amesema, hadi sasa ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 98.5 na limeanza kupitika.
Amesema,daraja la Nanjoka lilitakiwa kujengwa kwa muda wa miezi mitano,hata hivyo kutokana na jitihada za Tarura na uwezo wa mkandarasi kazi imekamilika katika kipindi kifupi.
Ngonyani ametaja kazi zilizobaki ni ujenzi wa mifereji upande wa kulia na kushoto urefu wa mita 300 na kuendelea kufukia mashimo sehemu chache kwa ajili ya kuimarisha daraja na barabara.
Ngonyani, amewataka wananchi kuzingatia sheria za utunzaji wa mazingira kwa kutofanya shughuli za binadamu ndani ya mita 30 kuanzia katikati ya mto ili kutoathiri miundombinu ya barabara zinazojengwa kwa fedha nyingi.
Kwa mujibu wa Ngonyani,kutozingatia sheria ya mazingira ndiyo sababu iliyopelekea hata daraja la awali kusombwa na maji kwani baadhi ya wananchi walitumia vibaya sehemu ya juu ya mto kufanya shughuli za kibidamu ikiwemo kilimo na ufugaji wa samaki jambo lililosababisha mto Nanjoka kupanuka.
“Tunduru tuna tatizo kidogo la wananchi kugeuza mifereji inayopitisha maji kuwa sehemu ya madampo,tunawaomba wananchi kuzingatia sheria za mazingira na kutunza barabara zinazojengwa kwa manufaa yao”alisema Ngonyani.
Alisema,kukamilika kwa daraja hilo la kisasa kunatoa fursa kwa wananchi kusafiri na kusafirisha mazao kutoka shambani kwenda sokoni na kusisitiza kuwa,ni muhimu kwa jamii kuhakikisha inatunza miudombinu inayojengwa kwa gharama kubwa.
Mkazi wa mtaa wa Majengo Saleh Haji,ameishukuru Serikali kujenga daraja la kudumu katika eneo hilo baada ya daraja la awali kusombwa na maji na kuleta adha kubwa kwao na kushindwa kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Alisema,daraja jipya ni bora tofauti na la zamani kutokana na kujengwa kwa viwango vikubwa hasa maeneo ya kupitishia maji chini ya daraja na kuwapongeza wasimamizi wa ujenzi huo wakala wa barabara za mijini na vijijini Tarura kwa kazi nzuri.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.