Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Mabula Misungwi Nyanda akiongozana na Maofisa waandamizi wa Taasisi hiyo amekutana na Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Simon Kemori Chacha kwa ajili ya kujadili mustakabali wa utatuzi wa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo inayowakabili wananchi wilayani humo.
Kamishna Mabula ameeleza namna Taasisi yake inavyotekeleza jukumu la kupambana na changamoto ya wanyamapori hao ili kuwaondolea adha wananchi na namna ilivyojipanga kutekeleza maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma Septemba, 2024 kuhusu kukabiliana na changamoto ya wanyamapori hao Katika wilaya za Tunduru na Namtumbo.
Mabula amesema TAWA inatarajia kuongeza vitendea Kazi ambapo Katika wilaya ya Tunduru itaongeza gari 1 na Pikipiki 2 zitakazotumiwa na Askari wahifadhi Kwa ajili ya mwitikio wa haraka wa matukio ya tembo, ikiwa ni pamoja na mabomu baridi 250 Kwa ajili ya kuwafukuza wanyamapori hao kutoka katika makazi ya watu.
Ili kuimarisha utendaji kazi, Kamishna Mabula amesema TAWA imejenga kituo cha Askari wa kudumu eneo la Chingulungulu na hivi karibuni itaongeza idadi ya Askari wahifadhi wapatao 20 Katika kituo kidogo cha Songea ili kuwaongezea nguvu Askari 8 waliopo sasa wilayani Tunduru ikienda sambamba na kuanzisha kituo cha muda cha Askari katika tarafa ya Namasakata.
Katika hatua nyingine Kamishna Mabula ametumia ziara hiyo kuongea na Maafisa na Askari wa uhifadhi ili kusikiliza changamoto wanazopitia Katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhimiza utendaji Kazi unaozingatia Sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kusisitiza ushirikiano na vyombo vingine vya dola hususani Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Simon Kemori Chacha amepongeza jitihada zinazofanywa na TAWA na Wizara ya Maliasili na Utalii Kwa ujumla wilayani humo Katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo na kusisitiza kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao Kwa wananchi
Pia ametilia mkazo suala la ushirikiano baina ya Halmashauri, Taasisi za uhifadhi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na wadau wa uhifadhi Katika kutekeleza Mkakati wa Wizara wa kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.