WAKAZI wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameshiriki katika Bonanza maalum la kuhamasisha wananchi wa wilaya hiyo na Watanzania kujiandaa kushiriki kikamilifu zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi huu nchini kote.
Bonanza hilo maarufu kwa jina la SAMIA SENSA BONANZA-TUNDURU limeshirikisha michezo mbalimbali ya matembezi ya hiari umbali wa km 7,mpira wa miguu,bao,drafti,mpira wa wavu,kukimbiza kuku na rede kwa wasichana ambapo washiriki wametoka kata zote 39 za wilaya ya Tunduru.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Bonanza hilo Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro,amewataka wananchi kujiandaa kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa na makazi ili kuiwezesha serikali kupanga maendeleo,kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa nchi yetu.
“matokeo ya sensa ya mwaka huu itasaidia serikali kupata taarifa na takwimu sahihi za wananchi wake na kupanga mipango ya maendeleo hasa ikizingatiwa kuwa, katika sensa ya mwaka 2012 wilaya yetu haikufanya vizuri kutokana na baadhi ya wananchi kutoshiriki zoezi hilo muhimu”alisema.
Amewaomba Wananchi, kutoe ushirikiano kwa watu waliopewa kazi ya kukusanya takwimu na taarifa mbalimbali ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kama ilivyopangwa na Serikali.
Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usalama amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani humo, kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa sensa kwa wananchi ili kuwaweka tayari kushiriki zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Amewashukuru wakazi wa Tunduru hasa vijana na watu wengine waliofika kushuhudia Bonanza la Samia Sensa-Tunduru lililofanyika katika uwanja wa michezo wa CCM Tunduru mjini kuacha shughuli zao na kushiriki katika Bonanza hilo.
Kwa mujibu wa Mtatiro,Bonanza hilo ni mwanzo wa kuanza kwa Ligi ya Samia Sensa Bonanza-Tunduru ambayo itafanyika kuanzia ngazi ya vijiji,kata,tarafa na baadaye ngazi ya wilaya ambayo itatumika kwa kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi pamoja na kuibua vipaji kwa vijana wa wilaya hiyo.Aidha katika Bonanza hilo, kulifanyika mechi ya hiari ya mpira wa miguu kati ya Timu Ditram Nchimbi na Timu ya mwanamuziki wa kizazi kipya Frank Ngumbuchi(FOBI) na Timu Ditram iliifunga Timu Fobi goli 1-0. goli lililofungwa na Ditram Nchimbi dk 80.
Kwa upande wake Ditram Nchimbi,amewaomba Watanzania kujiandaa kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi na kuwataka wana michezo na makundi mengine kuungana na Serikali kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hilo.
Alisema,sensa ya watu na makazi ni muhimu sana kwani serikali ina lengo la kupata taarifa sahihi za idadi ya watu wake ili iweze kupanga mipango na kutoa hudumu za kijamii.
Naye Nahodha wa Timu ya Fobi Frank Ngumbuchi(Fobi)alisema ataendelea kuiunga mkono serikali katika kufanikisha utekelezaji wa zoezi la sensa na kuwaomba wakazi wa Tunduru na mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kila mmoja anahesabiwa ili serikali iweze kupata takwimu sahihi na za uhakika wakati wa kupanga mipango ya maendeleo.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.