SERIKALI kupitia Hospitali ya wilaya ya Tunduru kitengo cha Kifua Kikuu na Ukoma, imezindua rasmi kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu mwaka 2022 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kutokana na kundi hilo kuwa katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo.
Katika kampeni hiyo yenye kauli mbiu “kila unayemuona mbele yako ni mhisiwa wa kifua kikuu” itaenda sambamba kwa kuwapima na kuwaanzia dawa watoto wote watakaobainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa TB.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa wilaya,Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,kampeni hiyo ni endelevu na lazima kwa watoto wote walio chini ya umri huo.
Dkt Kihongole alisema,wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru watazunguka kila kijiji kwa ajili ya kutoa elimu ya kifua kikuu,kufanya uchunguzi na kuwaanzishia matibabu watakaobainika kuwa na dalili za kifua kikuu.
Alisema, katika mkoa wa Ruvuma wilaya ya Tunduru inatajwa kuongoza kuwa na wagonjwa wengi wa kifua kikuu ambapo kwa mwaka 2021, jumla ya watu 769 waliobainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Alisema,kifua kikuu ni ugonjwa unaoambikizwa kwa njia ya hewa ambapo mtu mwenye ugonjwa huo anapokohoa bila kuziba mdomo ni rahisi sana kuwaambukiza wengine.Kihongole alitaja dalili za ugonjwa huo kwa watoto wadogo ni kupungua na kutoongezeka uzito,homa za mara kwa mara,kulia lia na makuzi duni
Amewataka wazazi na walezi, wanapoona dalili hizo kwa watoto ni vyema kuwapela Hospitali na vituo vya afya vilivyopo katika maeneo yao kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalam.
Aidha alitaja dalili kwa watu wazima ni kukohoa kwa muda wa wiki mbili na zaidi,kukohoa damu,kutoka jasho usiku wa manane,kukonda na kupoteza hamu ya kula.
Kihongole,ameyataja makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo ni watoto wadogo,wazee,watu wanaoishi na virusi vya ukimwi,wanaokunywa pombe kupita kiasi,wasafiri na wanaoishi na kukaa kwenye mikusanyiko kama wanafunzi wanaoishi bweni na wafungwa.
Amina Jinga,amepongeza jitihada za serikali katika kupambana na ugonjwa huo kwani zitawasaidia wazazi na walezi kufahamu afya za watoto wao na kuchukua hatua pale watakapobainika kupata na ugonjwa huo.
Secilia Komba,ameiomba Serikali kupitia wataalam wake kutembelea mara kwa mara maeneo ya vijijini kwa ajili ya kutoa elimu ya magonjwa mbalimbali ikiwamo TB kwa sababu maeneo mengi hayo wananchi hawana elimu ya kutosha kuhusu kifua kikuu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.