Na Albano Midelo
WILAYA ya Nyasa mkoani Ruvuma bado ina fursa za maliasili ya kutosha zikiwemo misitu, wanyamapori, samaki, mito, ziwa, fukwe na mali kale ambazo hazijaharibiwa ndiyo maana tunasema wilaya ya Nyasa ni benki ya vivutio vya utalii na uwekezaji.
Fursa hizo zinaweza kutoa mchango mkubwa kwenye pato la Taifa na wananchi wa wilaya ya Nyasa,mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla kupitia utalii wa kiutamaduni na ikolojia.
Makao makuu ya Wilaya ya Nyasa yapo katika Mji wa Mbambabay.wilaya hiyo ina sifa ya kuwepo kwenye bonde la ufa,ambapo bonde hilo huanza kuonekana kutoka katika maeneo ya Buruma, unaposhuka milima katika kona zinazoitwa Ambrosi.
Moja ya kivutio adimu cha utalii katika wilaya ya Nyasa ni uwepo wa Ziwa Nyasa ambalo linapatikana Kusini – Magharibi mwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Ziwa Nyasa ni la tisa kwa ukubwa duniani,ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika.
Ziwa hilo lina kina cha kati ya mita 426 na 758 na hii ni kutokana na kupitiwa na bonde la ufa. Kwa upande wa Tanzania mito mingi inapatikana ikitokea wilaya ya Nyasa katika safu za milima ya Livingstone, mito hiyo ni Ruhuhu, Lumeme, Ruhekei,Lwika,Mbamba Bay,Likumbo na Chiwindi ambayo huingiza maji ndani ya Ziwa Nyasa.
Zwa Nyasa ni kuvutio kikubwa cha Utalii kanda ya kusini kwa kuwa limesheheni vitu vingi ndani yake na tabia tofauti ukilinganisha na maziwa mengine ya hapa nchini na duniani kote.
Baadhi ya tabia za ziwa hili ni uwepo wa maji meupe na maangavu eneo lote la ziwa na mawe marefu ambayo yanajulikana kwa majina ya hia na mala yanayobeba sifa tofauti.
Tabia nyingine za Ziwa hilo ni mawimbi makubwa, fukwe nzuri na zenye sifa tofauti, mawe kuonekana kama sakafu eneo la Chiwindi, fukwe zenye udongo wa mfinyanzi, kina cha maji kuwa kifupi kwa umbali mrefu na mchanga mdogo ambao watu wa kale walitumia kusugulia meno ili yawe meupe hasa katika fukwe za Mtipwili.
Kulingana na ripoti ya utafiti wa mwaka 2011,asilimia 15 ya aina za samaki wa maji baridi duniani wanapatikana ziwa Nyasa ambapo kuna aina ya samaki tofauti zaidi ya 600,huku kukiwa aina ya samaki wa mapambo zaidi ya 400 na viumbe wengine ambao hawapatikani katika ziwa lolote duniani wanapatikana katika maeneo tofauti ndani ya ziwa Nyasa kutegemeana na aina na usalama wa maisha yao.
Jonathan Ruanda Mtaalam wa kuzamia samaki wa mapambo katika ziwa Nyasa na Mfanyabiashara wa samaki hao anasema tangu mwaka 1960 samaki hai wa mapambo walianza kuuzwa katika nchi za Ulaya na Marekani.
Hata hivyo anasema nchi nyingi kama vile Japani, Swedeni, Uturuki, Denmark, Canada, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zilivutiwa na samaki wa mapambo kutoka ziwa Nyasa kutokana na kuwa na sifa ya kipekee yaani rangi nzuri za kupendeza na hakuna sehemu nyingine wanapatikana samaki wa mapambo wa aina hii.
Afisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anabainisha kuwa Ziwa Nyasa pia limesheheni utajiri mkubwa wa viumbe hai wakiwemo fisimaji, mamba, nyoka na viboko ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.
“Ndege wanaohamia kutoka Ulaya na baadhi ya nchi za Afrika wanapatikana maeneo ya mwambao mwa ziwa Nyasa ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.Ndege hao huja kwa ajili ya kujipatia chakula cha aina mbalimbali katika mwambao wa ziwa Nyasa wakiwa kwenye misafara yao’’,anasisitiza Challe.
Akizungumzia jina la Mbambabay mji ambao ni makao makuu ya wilaya ya Nyasa,Challe anabainisha jina la “Mbamba bay,” kwamba Mbamba ikiwa na maana ya radi na bay ikimaanisha Ghuba na kwamba vyote hivyo ni vivutio vyenye historia ya kupendeza na kuvutia kwa wageni.
“Tafsiri hizi ambazo zilitolewa na wenyeji zinasema wakati wa zamani kutokana na radi kali za mara kwa mara kupiga kwenye Rasi iliyopo karibu na Ghuba hiyo na ndipo eneo likaitwa Mbamba bay’’,anasisitiza Challe.
Rasi hiyo ni kubwa na imefunikwa na uoto wa asili wa miti na nyasi ambapo baadhi ya miti hiyo inatumika kama dawa za asili hadi sasa.
Watu pia hutumia msitu wa Mbamba kwa matambiko ya kupiga ngoma za kufukuza au kuita majini kwa imani zao na kwamba katika msitu huo kuna wanyama kama chui wakitokea milima ya Nangombo, Ukuli na Chinyemba ambao wanapatikana katika rasi hiyo,wakiwafuata wanyama aina ya ngedere waliopo kwa wingi katika msitu huo.
Usikose sehemu ya pili ya Makala haya
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.