Utalii wa utamaduni ni eneo lingine ambalo linachangia sana kukuza utalii wa mahali popote,Watu walioishi miaka mingi iliyopita Wilaya ya Nyasa walicheza ngoma mbalimbali zikiwa na lengo la kuburudisha, kuelimisha, kukosoa au kuwapongeza watu mbalimbali waliofanya mambo mazuri kwa jamii.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa na Naibu Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Mhandisi Stella Manyanya anataja moja ya ngoma hizo ni Mganda,ngoma hii ilichezwa na wanaume na ngoma ya Kioda ambayo walicheza akina mama.Ngoma nyingine kama vile Lindeku, Mhambo, Lingoga na Chomanga walicheza mchanganyiko wanaume na wanawake.
Anasema katika utamaduni jamii za Nyasa zilialikwa kucheza ngoma za jadi nchi jirani za Msumbiji na Malawi, jambo ambalo hadi sasa bado linadumishwa la watanzania kualikwa kucheza ngoma Msumbiji au wa Msumbiji kualikwa Tanzania hasa vijiji vya mpakani kama vile Chiwindi.
Vyakula ni sehemu kubwa ya utalii,vyakula vya asili kwa wakazi wa Nyasa vimegawanyika katika makundi yafuatayo; chakula kikuu ni ugali wa muhogo, mahindi, ulezi, mtama na ngano, vitoweo vimegawanyika katika makundi manne yafuatayo ambavyo ni samaki wakubwa na wadogo Pamoja na na dagaa.
Kundi la pili ni mboga za majani ikiwemo mlenda, kisamvu, mchicha asili (libonongo), kundi jingine ni wadudu kumbikumbi, likungu, chenene (makururu), viyenje,mbambwa (majimoto) na manganiwa.
Wilaya ya Nyasa pia ina pori ya akiba la wanyamapori la Liparamba ambalo lina wanyama wengi wakiwemo tembo, simba, chui, nyati, ngolombwe, parahala, tandala wakubwa, pundamilia, nyani manjano, pongo, Ngiri, pofu, kuro, fisi, nguruwepori na ndege jamii mbalimbali zaidi ya aina 80 ambao ni kivutio kizuri kwa watalii.
Wanyamapori hao wa Liparamba katika majira fulani ya mwaka wanatabia ya kuhama kwenda nchi jirani ya Msumbiji na baadaye hurudi tena kwenye pori la Liparamba kwa kuwa eneo hilo ni ushoroba wa wanyamapori.
Liparamba pia ni pori lenye maporomoko ya maji ya mto Ruvuma ambao umepita humo na unapokea maji kutoka mito miwili ya Lunyele na Lumeme ni kivutio kikubwa cha utalii na uwekezaji katika sekta.
Wilaya ya Nyasa ili iendelee kuwa kitovu cha utalii mkoani Ruvuma,uongozi unaendelea kulinda maeneo ya kihistoria na kiutamaduni kwa kushirikisha wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.