Na Gustaph Swai-RS Ruvuma
Msajili wa Jumuiya za Kiraia kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani Emmanuel Kihampa ametoa wito kwa viongozi wa dini mkoa wa Ruvuma kuzingatia sheria,uwajibikaji na uwazi katika shughuli za uendeshaji wa Taasisi zao.
Kihampa ametoa rai hiyo wakati anatoa semina kwa viongozi wa Dini kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma kwenye ukumbi wa sekondari ya Songea Girls mjini Songea.
Amewaasa mesisitiza kutoa taarifa kwa Mamlaka husika pale wanapotembelewa na wageni na kueleza kuwa baadhi ya taasisi za dini zinaweza kutoa mianya bila kujua kwa vitendo vya kigaidi na uhalifu.
Msajili huyo amewaonya viongozi wa dini dhidi ya uanzishwaji holela wa vituo vya mafunzo ya kidini na kufafanua kuwa ni muhimu kufuata utaratibu wa kuanzisha vituo hivyo ili kulinda maadili na kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanawiana na dini husika na sheria za nchi.
"Taasisi za kidini ni muhimu kuzingatia maadili ya kazi za dini, kanuni na misingi ya Imani zenu na maadili ya Kitanzania, Ni jambo la kushangaza kiongozi wa dini kufanya vitendo visivyoendana na Mila na desturi za Kitanzania",alisisitiza.
Pamoja na hayo, Bw.Kihampa amewakumbusha viongozi wa dini umuhimu wa kuzingatia masharti ya usajili na matakwa ya sheria zote za nchi, na kusisitiza ushirikiano kati ya viongozi wa dini na vyombo vya serikali ili kudumisha amani na mshikamano.
Katika hatua nyingine Msajiri huyo ametoa onyo kali kwa viongozi wa dini kuhusu kutoa mahubiri yenye uchochezi wa kidini, kisiasa, au kikabila, ambapo amesisitiza viongozi wa dini wanapaswa kutumika kama wapatanishi na kuwaunganisha Watanzania, badala ya kuchochea migawanyiko.
Msajili amezionya taasisi za kidini ambazo zitabainika kwenda kinyume na maadili au kuashiria uvunjifu wa amani zinaweza kuchukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kufungiwa na mamlaka husika za serikali.
Ofisini ya Msajili wa Jumuiya za kiraia ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwa na wajibu wa kusajili na kusimamia taasisi zote za kidini nchini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.