MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewaongoza viongozi wa dini na wazee maarufu katika Mkoa wa Ruvuma katika maombi maalum ya kuombea Taifa kuelekea uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Maombi hayo yamefanyika katika viwanja vya Ikulu Ndogo mjini Songea ambapo baada ya maombi wazee na viongozi wa dini washiriki kula chakula cha jioni na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza kabla ya maombi hayo Mndeme amewashukuru viongozi wa dini na wazee maarufu kwa kumuunga mkono Rais Dkt.John Magufuli katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo amewashauri kuendelea kumuunga mkono ili maendeleo aliyoyaanzisha aweze kuyamalizia katika kipindi cha miaka mitano iliyobaki.
Amesema Rais Magufuli katika kipindi cha miaka mitano amefanikiwa kuwaunganisha watanzania wote kuwa kitu kimoja ambapo Rais Magufuli akiwa kanisani alianzisha michango ya ujenzi wa msikiti jambo ambalo amesema halijawahi kutokea katika historia ya Tanzania.
“Magufuli ni Rais ambaye amedhamiria kutuunganisha watanzania kwa hiyo tuna kila sababu ya kuendelea kumuunga mkono,ili kasi hii ya maendeleo aliyoianzisha kwa wananchi aweze kuikamilisha’’,alisema Mndeme.
Mndeme amewaasa wazee na viongozi wa dini kuendelea kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwa kila jambo na kuendelea kumuombea Rais Magufuli afya njema na maisha marefu sanjari na kufundisha mafundisho mema kwa vizazi vyote vitambue kazi njema inayofanywa na serikali ya awamu ya tano.
Amesema serikali ya Rais Magufuli inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa treni ya kisasa kutoka Mtwara hadi Mbambabay mkoani Ruvuma na kwamba watalaam wanafanya upembezi kwa ajili ya maandalizi ya mradi huo.
“Sisi wanaruvuma tutanufaika sana na miumbombinu hii ,unaweza kuamua kusafiri kwa gari,treni,meli na ndege ,nawaambia haya kwa sababu mimi nimeshiriki na nimeona taarifa ya awali ya ujenzi wa reli ya Mtwara hadi Mbambabay’’,alisema.
Kwa upande Mwakilishi wa viongozi wa dini Askofu Alimosa Mwasangapole wa Kanisa la TAG Songea amesema viongozi wa dini wanaridhishwa na kazi ambayo anaifanya Rais Magufuli kutambua mchango wa dini katika maendeleo ya Taifa.
“Nimekuwepo tangu wakati wa uhuru,nimeona marais wote lakini huyu mtu ni wa pekee,kwa namna Rais Magufuli anavyowajengea watanzania imani kuhusu Mungu,huyu angepewa tu udaktari wa dini’’,alisema Askofu Mwasangapole.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Manispaa ya Songea Exavery Nyoni akizungumza kwa niaba ya wazee wa Mkoa wa Ruvuma amesema isingekuwa Ilani ya CCM kupitisha mgombea Urais kufanya kazi kwa miaka kumi wangependa Rais Magufuli afanyekazi ya Urais katika maisha yake yote.
“Huyu nasema ni mtoto wa Nyerere kwa sababu yale yote ambayo Nyerere aliyaotea huyu ndiyo anayafanya,ingekuwa sio Ilani ya CCM tungesema aendelee tu mpaka Mungu atakapotaka,kwa kweli Mkoa wetu wa Ruvuma hadi sasa tumepiga hatua kubwa katika maendeleo’’,alisisitiza Nyoni.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Ikulu Ndogo Songea
Septemba 8,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.