MKAGUZI wa Mbolea kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)Christian Mhando ,ametoa onyo kwa wafanyabiashara wa mbolea kuhakikisha wanauza mbolea kwa bei elekezi kwa mbolea zote za kupandia na kukuzia.Katika Mkoa wa Ruvuma kuna kampuni saba za kununua mbolea na mawakala wa mbolea zaidi ya 120
Mhando ametoa onyo hilo wakati anakagua maghala ya kuhifadhia mbolea na mawakala wanauza mbolea katika maduka mbalimbali mkoani Ruvuma.
“Wafanyabiashara hao wahakikishe wanatoa risiti za mashine mara baada ya kuuza mbolea hizo kwa wananchi,pia wauze mbolea ambazo zimesajiriwa na TFRA na kuzingatia utunzaji bora wa mbolea kwa kuwauzia wakulima mbolea zenye ubora,na yeyote atakayekwenda kinyume na maelekezo hayo atachukuliwa hatua’’,alisisitiza Mhando.
Mkaguzi huyo wa mbolea amewatahadhari wafanyabiashara kuacha tabia ya kuuza mifuko ya mbolea ambayo imefunguliwa ambapo anasema TFRA itachukua hatua Kali ikiwemo kuwanyang’anya leseni,kufunga biashara na kupelekwa mahakamani ili kufunguliwa mashitaka kwa mujibu wa sheria ya mbolea.
Hata hivyo amesema imebainika baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wanakiuka bei elekezi ya mbolea kwa kuongeza bei na kwamba changamoto hiyo imekuwa inajitokeza zaidi ya kwa wafanyabiashara wadogo ambapo amezipongeza kampuni za uuzaji wa mbolea kwa kuzingatia bei elekezi na kwamba baadhi ya Kampuni zimekuwa zinauza chini ya bei elekezi hivyo kuleta unafuu kwa wakulima.Mhando amesema kutokana na changamoto hizo kila mwaka wamekuwa wanakutana na wadau wa mbolea wakiwemo wawakilishi wa wakulima,wafanyabiashara wa mbolea na kampuni za mbolea ambapo wanapanga bei kwa pamoja na kuridhiwa na Waziri wa Kilimo kisha kutangaza bei elekezi.
Amesisitiza kuwa bei elekezi za mbolea za Tanzania zimekuwa rafiki kwa wakulima ukilinganisha na nchi nyingine hasa katika kipindi hiki cha janga la corona ambapo imebainika bei ya mbolea ya Tanzania ni ya chini zaidi hivyo kuleta unafuu kwa wakulima.
“Ukiangalia katika Mkoa wa Ruvuma katika msimu huu,mbolea ya kupandia bei yake haitazidi shilingi 50,000 kwa mfuko na mbolea ya kukuzia itakuwa kati ya shilingi 46,000 hadi 47,000 itategemea na mazingira ambayo mkulima yupo’’,alisema Mhando.
Mkaguzi huyo wa Mbolea wa TFRA amesema serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kujitahidi kuhakikisha kuwa bei ya mbolea kwa mkulima inaendelea kupungua na kwamba awali mfuko mmoja wa mbolea ulifikia zaidi ya shilingi laki moja ambapo hivi sasa imeshuka hadi kufikia chini ya shilingi 50,000.
Alisisitiza kuwa mbolea ya Tanzania inauzwa kwa gharama nafuu hali inayosababisha wakati mwingine wafanyabiashara kutorosha mbolea hiyo kwenda kuuza katika nchi za jirani.
Mhando anabainisha zaidi kuwa mbolea inapoingizwa nchini ,serikali ya awamu ya Tano imeondoa tozo zaidi ya 114 ambazo zilikuwa zinaathiri wakulima hali ambayo imesababisha bei ya mbolea kuendelea kupungua.
Kwa upande wake Afisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Onesmo Ngao ametoa rai kwa wakulima kuhakikisha wananunua mbolea yenye ubora na hasa katika kipindi hiki ambacho tayari serikali imetoa bei elekezi ya mbolea katika Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Ngao ameyataja mahitaji ya mbolea katika katika Mkoa wa Ruvuma kwa msimu ujao wa 2020/2021 kuwa ni tani 50,000 na kwamba serikali inaendelea kuhimiza kampuni za mbolea kuingiza mbolea ambapo hadi sasa mbolea ambayo imeingizwa katika Mkoa wa Ruvuma ni zaidi ya tani 3,500 na juhudi za kupeleka mbolea vijijini kwenye wakulima wengi zinaendelea.
Ametoa rai kwa wakulima mkoani Ruvuma katika kipindi hiki cha uuzaji wa mazao kununua mbolea kwa ajili ya matumizi ya msimu ujao wa kilimo ambapo hivi sasa maduka mengi yanauza mbolea chini ya bei elekezi.
Katika msimu wa mwaka 2019/2020 Mkoa wa Ruvuma ulilima hekta 268,008 za mazao mbalimbali zilizotoa mavuno ya Tani 787,321 hii ni sawa na ongezeko la Tani 50,628.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Septemba 6,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.