Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Peres Magiri, amewataka watumishi kuzingatia misingi ya utawala bora ili kuondoa kero katika utumishi na kuondoa migogoro kati ya waajiri na wafanyakazi.
Ametoa wito huo wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, ambayo kimkoa yamefanyika katika uwanja wa Majimaji manispaa ya Songea.
"Jambo moja ambalo litatusaidia kuondoa kero katika utumishi ni kuzingatia misingi ya utawala bora, utawala bora si tu husaidia kutatua kero za wafanyakazi, pia huepusha mikwaruzano na migogoro kati ya mwajiri na mfanyakazi, na uzoefu unaonyesha kuwa migogoro ya wafanyakazi na waajiri hujitokeza ambapo kanuni za utawala bora za ushirikishwaji, uwajibikaji na uwazi hazifuatwi," alisema Mhe. Magiri.
Amebainisha kuwa Serikali inatambua kuwa wafanyakazi wamekuwa na mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo wananchi.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Magiri amewataka waajiri na wafanyakazi kushirikiana ili kuhakikisha vyanzo vinavyosababisha kero, changamoto na migogoro katika utumishi vinazuiwa ili kuleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla huku Serikali ya Awamu ya Sita ikiendelea kufanyia kazi changamoto za wafanyakazi na maslahi ya wanaostaafu na wanaotarajia kustaafu.
Naye Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoa wa Ruvuma (TUCTA), Arab Bakari, amesema kama vyama vya wafanyakazi wanakemea vikali watumishi wasiowajibika, wabadhilifu wa mali za umma, wazembe, wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na unywaji wa Pombe kupindukia katika maeneo ya kazi kwa kuwa ni vitendo visivyokubalika katika utumishi wowote.
Kila mwaka, tarehe 1 Mei, dunia huadhimisha Siku ya Wafanyakazi, ikiwa ni fursa ya kuwakumbuka na kuwapa heshima wale waliojitokeza kwa ujasiri kupinga manyanyaso na ukiukwaji wa haki za binadamu. Wafanyakazi hao wa awali walipambana dhidi ya unyonyaji wa mabepari katika kipindi cha Mapinduzi ya Viwanda na Kilimo mnamo Karne ya 18, wakitaka mazingira bora ya kazi na haki zao kutambuliwa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.