WANANCHI wa jamii ya kifugaji wilayani Tunduru,wameiomba serikali kuwasogezea huduma za afya ikiwemo za uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu katika maeneo yao ili kuepusha uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa huo.
Wametoa ombi hilo jana,kwa wataalam wa kitengo cha kifua kikuu na ukoma kutoka Hospitali ya wilaya Tunduru wakati wa kampeni ya uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwa jamii ya wafugaji wanaoishi katika kijiji cha Mkowela wilayani humo.
Samwel Mandalu(65) alisema,wakati umefika kwa serikali kutoa upendeleo kwa kuwajengea zahanati katika maeneo yao ili waweze kupata huduma za afya ikiwemo uchunguzi wa ugonjwa kifua kikuu.
Alisema,kutokana na mazingira na shughuli zao kufanyika mbali na makazi ya watu wengine inakuwa vigumu kufikiwa na elimu ya afya mara kwa mara.Alisema,watashukuru iwapo serikali itapeleka huduma za afya kwenye maeneo yao ili iwe rahisi kupata elimu juu ya ugonjwa wa kifua kikuu na magonjwa mengine.
Alisema kuwa,wafugaji wengi wanaishi kwenye vitalu maeneo ya porini ambako wanategemea dawa za asili tu kama tiba ya maradhi yao huku baadhi yao hawajawahi kukutana na wataalam wala kufika Hospitali katika maisha yao yote.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa zahanati ya Mkowela Dkt Neema Msangilwa alisema,kwa mwaka 2022 walifanikiwa kuibua wagonjwa 100 wa kifua kikuu.
Alisema,wagonjwa hao walipatikana kupitia kampeni mbalimbali zinazofanyika na wengine walipatikana kupitia dalili zinazoonyesha wanapofika zahanati kwa ajili ya kupata matibabu.
Alisema kijiji cha Mkowela kina zaidi ya watu elfu mbili,hivyo watu 100 wenye kifua kikuu ni wengi mno,ambapo ameiomba serikali kuendelea kufanya kampeni hizo mara kwa mara ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.