JUMLA ya kilo 308,774 za korosho kutoka vyama vya msingi vya ushirika vinavyosimamiwa na Chama Kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru (Tamcu Ltd), zimeuzwa katika mnada wa 10 uliofanyika katika ghala la TAMCU Tunduru mjini.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika(Tamcu)wilayani Tunduru Imani Kalembo alisema, katika mnada huo kampuni moja ya RV Export Ltd ndiyo imejitokeza kuomba kununua ambapo korosho daraja la pili ziliuzwa kilo 151,440 kwa bei ya sh.1,340 kwa kilo moja na daraja la kwanza zimeuzwa kilo 157,334 kwa sh.1,600.
Alisema,hadi sasa Chama Kikuu kimeshafanya minada 9 na jumla ya tani 14,380 zenye thamani ya Sh.bilioni 25 zimekusanywa na kuuzwa kwa makampuni mbalimbali.
Hata hivyo alieleza kuwa,kiasi hicho cha korosho zilizozalishwa katika msimu 2022/2023 ni nusu ya uzalishaji msimu wa mwaka 2021/2022 kwani katika msimu uliopita wakulima walifanikiwa kuzalisha na kuuza zaidi ya tani 25,000.
Kalembo,amewaasa wakulima ambao bado wana korosho majumbani,kuhakikisha wanapeleka kwenye vyama vyao vya msingi(Amcos) kwa ajili ya kuuza ili kuwahi mnada wa mwisho utakaofanyika wiki ijayo.
Aidha,amewataka kufanya palizi ya mashamba yao na kutumia fedha wanazopata kununua pembejeo za ruzuku zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita,na kuepuka kutumia kwenye mambo ya anasa jambo linaloweza kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Makamu mwenyekiti wa Tamcu James Chipojola alisema,uzalishaji mdogo wa korosho katika msimu wa mwaka huu umeathiriwa sana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo mvua za masika ziliwahi kunyesha na hivyo kuathiri sana uzalishaji na kupunguza ubora wa korosho.
Chipojola,amewashauri wakulima ambao ni wanachama wa Tamcu, kuanza kulima mazao mengine ya biashara kama vile ufuta,mbaazi,soya, na alizeti ili kujiongezea kipato,badala ya kutegemea zao moja tu la korosho ambalo kwa sasa linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya bei.
Naye Afisa ushirika wa wilaya hiyo George Bisani alisema, katika msimu wa 2022/2023 malengo yalikuwa kuzalisha tani 30,000 lakini hawawezi kufikia kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo mashambani.
Bisani,amewaomba wakulima kutokata tamaa kutokana na changamoto zilizojitokeza katika msimu huu,bali waendelee kufanya maandalizi ya msimu mpya kwa kupalilia mashamba yao na kufuata ushauri wa wataalam wa kilimo.
Mmoja wa wakulima wa zao hilo Issa Lada,ameiomba serikali kusimamia bei ya korosho kwani wakulima wanatumia gharama kubwa katika uzalishaji,lakini bei zinazotolewa na makampuni yanayonunua korosho ni ndogo na hailingani na gharama za uzalishaji wake.
Alisema,kama serikali itajipanga na kusimamia vizuri suala ya bei kwa zao la korosho uchumi wa wilaya hiyo utakuwa mkubwa na wakulima watapata fedha nyingi na kuongeza uzalishaji mashambani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.