WAKAZI wa kata ya Myangayanga katika Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wanatarajiwa kuondokana na kero ya kutembea zaidi ya kilomita 7 kwenda hadi Mbinga mjini kufuata huduma za matibabu kufuatia serikali kuwa katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa kituo cha Afya kitakachogharimu kiasi cha Sh.milioni 225,000,000.
Hayo yamesemwa na Kaimu Afisa Mtendaji wa kata hiyo Amos Ndomba alipokuwa akitoa taarifa ya ujenzi kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim.
Ndomba alisema,Halmashauri ya mji Mbinga ilipokea fedha hizo kutoka serikali kuu na utekelezaji wa kituo hicho ulianza rasmi mwezi Oktoba mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 mwezi huu.
Alisema, fedha za awamu ya kwanza zimetumika kujenga jengo la maabara na jengo la wagonjwa wa nje(OPD) na majengo hayo yanajengwa kwa mfumo wa force akaunti.
Kwa mujibu wa Ndomba, hadi sasa mradi huo umefikia hatua ya kufunga milango na madirisha na fedha zilizotumika ni kiasi cha Sh.milioni 218,601,899.00 na kubakiwa na Sh.milioni 40,978,101.00 ambazo zitatumika kukamilisha kazi zilizobaki.
Alisema,wananchi wameshiriki katika ujenzi wa kituo hicho kwa kuchana mbao 2248 zenye thamani ya Sh.milioni 8,660,500,kusafisha eneo Sh,milioni 100,000,kuchimba msingi Sh.100,000,kulipa fidia ya eneo Sh.500,000 na wadau wengine wamechangia fedha taslimu kiasi cha Sh.220,000.
Aidha alisema,mradi huo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali wakati wa utekelezaji ikiwemo uhaba wa maji kipindi cha kiangazi na kusababisha ujenzi kusimama mara kwa mara hadi maji yalipopatikana na mvua kubwa iliyonyesha mwezi Disemba ilisababisha wananchi kushindwa kusomba mbao kutoka msituni.
Alisema,ujenzi wa kituo cha afya Myangayanga ukikamilika utasaidia sana kupungua kwa rufaa za wagonjwa kutoka zahanati za jirani kwenda Hospitali ya Halmashauri ya Mji,kupunguza adha kwa wananchi ya kufuata huduma za afya umbali mrefu.
Alitaja faida nyingine za mradi huo ni pamoja na kuongezeka kwa huduma za kiuchunguzi kupitia maabara,kuwepo kwa huduma za upasuaji kwa akina mama wajawazito na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama na watoto.
Mwenyekiti wa kijiji cha Myangayanga Aidan Mwingira,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kutoa fedha za kujenga kituo cha afya Myangayanga na viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa kwa ushauri na usimamizi wao.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge mwaka 2023 Abdalla Shaibu Kaim,amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Mbinga Grace Quintine, kwa kazi nzuri ya kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kusogeza na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Mbinga.
Kiongozi huyo wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2023,ametoa wiki mbili kwa Halmashauri ya mji Mbinga kukamilisha ujenzi wa kituo hicho ili wananchi waanze kupata huduma za matibabu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.