Na Albano Midelo,Songea
WANAWAKE Zaidi ya 9,500 kati ya 100,000 hugundulika kila mwaka kuwa na tatizo la saratani ya mlango wa kizazi,kati yao wanawake 6,500 hufariki dunia kila mwaka.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Louis Chomboko wakati anatoa taarifa ya maadhimisho ya wiki ya chanjo na uzinduzi wa dozi moja ya chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Dr.Chomboko amesema inakadiriwa wanawake Zaidi ya 450,000 wamethibitika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi duniani na wengi wao wapo katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
“Saratani ya mlango wa kizazi inashika nafasi ya pili kwa kusababisha saratani kwa wanawake ulimwenguni,nafasi ya kwanza inashikwa na saratani ya matiti’’,alisisitiza.
Hata hivyo Dr.Chomboko amesema hapa nchini saratani ya mlango wa kizazi inaongoza miongoni mwa saratani zote zinazogundulika miongoni mwa wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 44.
Ameyataja mambo yanayochochea kupata saratani ya mlango wa kizazi kuwa ni kuanza kujamiana katika umri mdogo,kuwa na wapenzi wengi,kuwa na ndoa za mitaala,uvutaji sigara,kuwa na mpenzi asiyetahiriwa na virusi vya UKIMWI na UKIMWI.
Amezitaja dalili za saratani ya mlango wa kizazi kuwa ni kutokwa damu bila mpangilio,maumivu ya mgongo,kuchoka,kutoka uchafu kwenye uke, kuishiwa damu,figo kushindwa kufanya kazi, uvumbe wa tezi na kupatwa na fistula.
Baadhi ya wadau wa maendeleo mkoani Ruvuma wakiwa kwenye maadhimizo ya uzinduzi wa wiki ya chanjo mkoani Ruvuma
Ili kujikinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi,Mganga Mkuu huyo wa Mkoa wa Ruvuma amesema ni vema kupata chanjo ya kuzuia saratani hiyo,kubadili tabia,kuepuka ngono katika umri mdogo,kuepuka uvutaji sigara na kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu.
Akizungumzia huduma za kupima na kutibu saratani ya mlango wa kizazi katika Mkoa wa Ruvuma,Dr.Chomboko amesema Mkoa una jumla ya vituo 59 vinavyotoa huduma ya upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi na kwamba kati ya hivyo vituo 30 vina mashine za matibabu ya saratani ya mlango wa kizazi.
Amesema katika mwaka 2023,jumla ya wanawake 13,825 walichunguzwa na kati yao wanawake 348 waligundulika kuwa na viashiria vya awali vya saratani ya mlango wa kizazi na kwamba wanawake 313 walipatiwa tiba na wanawake 119 walihisiwa kuwa na saratani ya mlango wa kizazi.
Hata hivyo amesema wanawake 70 walithibitika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi ambao walipata rufaa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza kabla ya kuzindua maadhimisho hayo amesema Mkoa wa Ruvuma unatarajia kutoa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi 14 wapatao 147,447.
Ameitaja kaulimbiu ya wiki ya chanjo mwaka 2024 kuwa ni Jamii iliyopata chanjo yenye afya ambapo ametoa rai kwa jamii nzima kuhakikisha walengwa wote wanapata fursa ya kupata chanjo hiyo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge ametoa rai kwa viongozi wa dini na watendaji katika ngazi zote kuendelea kuwahamasisha wazazi na walezi wenye Watoto walengwa ambao bado hawajapata chanjo hiyo kuhakikisha Watoto wao wanapata chanjo hiyo muhimu.
Chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi mkoani Ruvuma imeanza kutolewa kuanzia Aprili 22 na inatarajia kukamilika Aprili 28 mwaka huu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.