Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezindua Mradi wa Kutatua migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika ukanda wa Ruvuma.
Uzinduzi wa mradi huo unaotekelezwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Shirika la (GIZ) la nchini Ujerumani umefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea ukishirikisha wawakilishi kutoka mikoa ya Ruvuma na Lindi.
Akizungumza kabla ya kuzindua mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amesema migongano baina ya binadamu na wanyamapori ni miongoni mwa changamoto kubwa katika mikoa ya kusini hivyo kuhatarisha Maisha ya wananchi na mali zao.
“Takwimu za mwaka mmoja pekee 2022/2023 zinaonesha kuwa wanyamapori wamesababisha vifo 35,majeruhi 17 na kuharibu takriban jumla ya hekari 10,724.05 za mazao mbalimbali ‘’’.alisema Kanali Thomas.
Hata hivyo amesema serikali ina matarajio kuwa mradi huo ambao utatekelezwa kwa kuhusisha Jeshi la Uhifadhi wa Misitu na wanyamapori kutoka TANAPA,TFS na TAWA Pamoja na mikoa na wilaya utapunguza au kumaliza changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori.
Ameagiza mara baada ya uzinduzi huo yafanyike maandalizi ya mpango mkakati utakaoanisha mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo pia amelipongeza Shirika la GIZ kwa kukubali kuleta mradi huo katika ukanda wa Ruvuma na kwamba mradi umekuja wakati muafaka kutokana na ongezeko la matukio la wanyamapori wakali na waharibifu.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Nchini Antonia Rafael akizungumza kwenye uzinduzi huo,amesema Mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Namtumbo na Tunduru mkoani Ruvuma na wilaya ya Liwale mkoani Lindi.
Amesema kutokana na kuongezeka kwa migongano baina ya binadamu na wanyamapori serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Amebainisha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imeingia mkataba wa kushirikiana na Shirika la GIZ la nchini Ujerumani ili kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika wilaya tatu za Tunduru,Namtumbo na Liwale kwenye mikoa ya Ruvuma na Lindi.
Amesema mradi huo unatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 hadi 2025 na kwamba mradi unagharimu zaidi ya bilioni 15.
Naye Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi wa TAWA Kanda ya Kusini Keneth Sanga amezitaja wilaya zinazoongoza kwa matukio mengi ya kuvamiwa na wanyamapori ambapo katika kipindi cha mwaka huu wilaya ya Lindi inayoongoza kwa kuwa na matukio 161,ikifuatiwa na wilaya za Nachingwea,Liwale,Rufiji na Tunduru.
Amewataja wanyamapori wanaohusika kwenye matukio hayo kuwa ni tembo anayeongoza kwa kusababisha matukio mengi ambapo kwa mwaka huu pekee tembo amesababisha matukio 682 akifuatiwa na simba, Nyati,kiboko,fisi na mamba.
Miongoni mwa maazimio yaliyopitishwa kwenye uzinduzi huo ni Pamoja na kuandaa mapema mpango shirikishi wa utekelezaji wa mpango huu ili kutatua changamoto hiyo katika ukanda wa Ruvuma.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.