Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma wilayani humo,imefanikiwa kuwabaini wagonjwa 389 wa kifua kikuu kati ya wahisiwa 7,354 waliofanyiwa uchunguzi wa ugonjwa huo kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2023.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole ameeleza, wagonjwa 200 wameibuliwa kati ya mwezi Januari hadi Machi na wagonjwa 189 wamepatikanakuanzia mwezi April hadi Juni.
Dkt Kihongole amefafanua kuwa,kati ya wagonjwa 389,watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na tano walikuwa 107 ambapo katika robo ya kwanza ya mwezi Januari-Machi wamefanikiwa kuwaibua watoto 52 na robo ya pili ya mwezi April -Juni watoto walioibuliwa ni 55.
Dkt Kihongole amesema hayo jana ofisini kwake,wakati akitoa taarifa ya hali ya maambukizi na mapambano ya ugonjwa huo kupitia kampeni zinazofanyika za kutokomeza ugonjwa huo katika kipindi cha miezi sita.
Amesema kati ya wagonjwa 389 waliokutwa na maambukizi ya Tb,wagonjwa 286 wamepatikana kutokana na mchango mkubwa wa jamii wakiwemo wahudumu wa afya ngazi ya jamii waliopata mafunzo maalum ya kupambana na ugonjwa huo.
Ametaja kazi zinazofanywa na wahudumu hao ni kupita nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kutoa elimu ya kifua kikuu kwenye jamii,kushiriki kwenye kampeni mbalimbali na kukusanya sampuli za makohozi kutoka kwa wahisiwa na kuzipeleka kwenye zahanati na vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi.
Kihongole amelitaja kundi lingine ni waganga wa tiba asili/tiba mbadala ambao wanakubalika na kuaminika sana kwenye jamii na pia wana wateja wengi kwenye maeneo yao ya kazi(vilinge).
Amesema,baada ya kutambua mchango wa waganga wa tiba asili katika mapambano ya kifua kikuu,Hospitali ya wilaya kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma imewapatia elimu ya kutambua dalili,unavyoambukiza na namna ya kujikinga ili wasipate ugonjwa huo .
Aidha, kundi lingine ni vyombo vya Habari ambapo jamii inapata uelewa wa kukabiliana na ugonjwa huo kupitia taarifa zinazochapishwa na kutangazwa kupitia wataalam wa afya kitengo cha kifua kikuu.
Aliongeza kuwa,wagonjwa wengi waliokutwa na maambukizi ya ugonjwa huo ni watu wanaoishi katika mazingira hatarishi kama vile wazee,waliopo kwenye misongamano na wanaoishi kwenye nyumba zilizokosa mwanga na hewa ya kutosha.
Amesema,Halmashauri ya wilaya Tunduru kupitia ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya kitengo cha kifua kikuu na ukoma kwa mwaka 2023 imepewa malengo ya kuibua wagonjwa 1,045 ambapo kila baada ya miezi mitatu wanatakiwa kuwapata wagonjwa 261.
Amesema,kupitia kampeni zinazofanyika mara kwa mara idadi ya wagonjwa inazidi kupungua na kama idara ina wapa matumaini kwamba elimu inayotolewa inawafikia walengwa ikilinganishwa na hapo awali.
Amesema,mwaka 2023 wamejipanga kuwafikia wagonjwa wote waliopo majumbani ili waendelee kumeza dawa na kuwaibua wagonjwa wapya kupitia kampeni zinazofanyika ili na kuwaanzishia matibabu.
Muhudumu wa afya ngazi ya jamii kutoka kikundi cha watu waliougua kifua kikuu na kupoma wilayani Tunduru(Mkikutu) Mungummoja Hyera alisema,wameamua kushirikiana na serikali katika kampeni hizo ili kwa pamoja waweze kutokomeza ugonjwa huo wilayani Tunduru.
Amesema,kazi kubwa wanayofanya ni kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu waliopo majumbani,hata hivyo changamoto kubwa katika kufanikisha lengo hilo ni suala la usafiri ili kuwafikia watu wengi hasa wanaoishi maeneo vijijini.
Katibu wa kikundi hicho Salum Kalembo alisema,wanatoa elimu,kuhamasisha na kuibua wagonjwa walioko majumbani ili waweze kwenda Hospitali kupata matibabu na kuokoa maisha yao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.