JUMLA ya watu 45,076 wamejitokeza kupima kwa hiari virusi vya UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma katika kipindi cha mwaka 2019.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Evance Nachimbinya wakati anatoa taarifa ya utekelezzji wa shughuli za kudhibiti maambukizo dhidi ya virusi vya UKIMWI kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme mjini Namtumbo.
Nachimbinya amesema kati ya waliopimwa watu 587 waligundulika kuwa na maambukizi na kwamba kiwango cha maambukizi katika Halmashauri hiyo kimepungua kutoka asilimia mbili mwaka 2018 hadi asilimia moja mwaka 2019.
Hata hivyo amesema katika kipindi hicho wanaume ndiyo wamejitokeza kwa wingi kupima kwa hiari ambapo jumla ya wanaume 30,303 walipima kwa hiari ukilinganisha na wanawake waliokuwa 14,773.
“Wote waliobainika kuwa na maambukizi walisajiliwa katika vituo vya tiba na matunzo kwa ajili ya usimamizi wa afya zao ili kuimarisha afya zao na wapate nguvu za kuendelea kulitumikia Taifa’’,alisisitiza Nachimbinya.
Ameyataja mafanikio ambayo Halmashauri hiyo imeyapata katika kukabiliana na UKIMWI kuwa ni kutoa huduma ya tiba na matunzo kwa waishio na VVU,upimaji kufanyika katika ngazi zote za kutolea huduma za afya ili kufikia malengo ya 95 tatu kufikia mwaka 2025 na kuendelea kwa huduma ya tohara kwa wanaume.
Licha ya mafanikio hayo,amezitaja changamoto zilizojitokeza katika kipindi hicho kuwa ni kupungua kwa mchango wa wadau kutokana na kupungua kwa bajeti ya Mfadhili Mkuu kwa serikali na changamoto ya usafiri katika vituo husika kutokana na Halmashauri kuwa na upungufu mkubwa wa magari.
Katika kukabiliana na changamoto hizo,Mkurugenzi huyo amesema Halmashauri inashirikiana na wadau wa shughuli za UKIMWI kama USAID BORESHA AFYA,NICE na ZHARF katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kuhakikisha kuwa Namtumbo inakuwa salama katika maambukizi mapya ya UKIMWI.
“Wilaya ina Kamati za kudhibiti UKIMWI katika kata 21 na vijiji 66,jumla ya kata zinazofadhiliwa na ZHARF zipo kumi,Halmashauri imeunda vikundi 14 vya watu waishio na virusi vya UKIMWI ambavyo vinashiriki katika uhamasishaji jamii juu ya kupima kwa hiari na utoaji elimu namna ya kujikinga na maambukizi ‘’,alisema Nachimbinya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akizungumza mara baada ya kukagua utekelezaji wa shughuli za kudhibiti maambukizi dhidi ya virusi vya UKIMWI wilayani Namtumbo,amewapongeza wanaume kwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao.
Mndeme amesema kitendo hicho kitaiwezesha serikali kufikia malengo yaliyopangwa ya kuwa na jamii salama kutokana na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kumaliza kabisa maambukizi.
“Hadi sasa jamii ya Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ina uelewa wa kutosha juu ya masuala ya VVU na UKIMWI,inatambua madhara yatokanayo ya unyanyapaa na inashiriki kikamilifu katika huduma zinazotolewa za upimaji na ushauri nasaha’’,alisema Mndeme.
Hata hivyo amesisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana,yanaonesha kuwa jitihada zikiendelea kuchukuliwa na wadau wote wa masuala ya UKIMWI,Wilaya ya Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla,utafikia malengo ya serikali ya kuwa na maambukizo sifuri ifikapo mwaka 2030.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 15,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.