WATUMISHI wa kituo cha Afya Kalembo Halmashauri ya Mji Mbinga,wameishukuru serikali kwa kuwajengea nyumba bora za kuishi na kueleza kwamba zimewaongezea morali ya kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi wanaofika kupata matibabu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti watumishi hao wamesema,nyumba hizo zimewafanya kuipenda kazi yao kwa sababu zimewaondolea msongo wa mawazo na changamoto ya mahali pa kuishi,tofauti na awali walipokuwa wamepanga nyumba mitaani ambazo hazikuwa na sifa ya kuishi mtumishi wa umma.
John Mtinda amesema,kutokana na mazingira ya ardhi la eneo hilo kuwa na tope jingi hasa nyakati za masika, ilikuwa vigumu kwao kufika kwa wakati inapotokea dharura ya kuhitajika kazini kuhudumia wagonjwa baada ya muda wa wakati kutokana na ubovu wa barabara kutoka kwenye makazi yao hadi kazini.
Amesema, kujengwa kwa nyumba hizo ni faraja kubwa kwao kwani zimesaidia sana kupata mahali pazuri na uhakika pa kuishi na kuhaidi kuzitunza nyumba hizo na kuongeza morali ya utendaji wa majukumu yao ya kila siku.
Ameipongeza serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Halmashauri ya Mji Mbinga,kujenga nyumba hizo karibu na eneo la kazi na kueleza kuwa,zimemaliza kabisa changamoto ya mahali pa kuishi kwa watumishi wa kituo hicho.
Mariam William mtaalam wa maabara amesema, kabla ya nyumba hizo walikuwa wanateseka kuhudumia wagonjwa hasa nyakati za usiku kutokana na kuishi mbali na eneo la kazi,lakini sasa wanapata muda wa kutosha na wanafika kwa wakati hata inapotokea dharura ya kuhitajika kazini.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Mbinga Maximo Magehema amesema,mpango wa Halmashauri ya Mji Mbinga ni kuhakikisha kila kinapojengwa kituo cha afya kunakuwa na nyumba ili kuwawezesha watumishi kuishi jirani na eneo la kazi ili waweze kutoa huduma kwa wakati.
Amesema,mpango huo ni endelevu kwa sababu utasaidia watumishi wa afya wanaoletwa na kufanya kazi katika Halmashauri ya mji Mbinga kuwa na mazingira mazuri,kuipenda kazi yao na kutojutia kuwepo katika Halmashauri hiyo.
Amewataka wananchi,kuendelea kutumia zahanati,vituo vya afya na Hospitali zilizopo na zinazoendelea kujengwa kwenda kupata huduma za matibabu kwa sababu serikali inajenga miradi hiyo kwa lengo la kusogeza na kuboresha huduma kwa wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.