Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amefanya ziara ya ukaguzi katika Kituo cha Ununuzu wa Mahindi cha Kizuka, Mkoani Ruvuma.
Akiongea na wakulima waliokuwa wanachekecha na kuchambua mahindi katika Kituo hicho, Waziri Bashe amewaeleza wakulima hao kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ni sikivu na imeweka kipaumbele katika kutatua changamoto zozote walizonazo kabla ya msimu wa mvua kuanza.
Wakulima kadhaa walieleza changamoto zao wakiwemo Bw. Nicodem Mayo, Bi. Zena Zawamba, Bw. Paul Philemon Haule na Baltazari Komba Mjinga, ambao wamevuna magunia zaidi ya 330 kwenye mashamba ya hekari 15 wameomba mawakala wanunue mahindi vijijini kwa angalau shilingi 600 hadi 650 badala ya shilingi 350 ambayo ni hasara kwa wakulima. Pia wameomba miundombinu ya barabara na mawasiliano kutengenezwa, mashine za kisasa kuchambua mahindi, kuongezewa huduma za maafisa ugani na zana za kilimo na mbegu bora.
Akijibu changamoto kadhaa, Waziri Bashe ameeleza kuwa “nimeona uhitaji wa kuwa na mashine ya kisasa ya kuchambua na kusafisha mahindi. Nimeielekeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua mashine za kisasa za kuchambua mahindi ili kurahisisha huduma za Kituo hicho kwa wakulima,” amesema Waziri Bashe.
Aidha, amemuomba Mkuu wa Wilaya Mhe. Wilman Kapenjama Ndile kutembelea mawakala wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na kuhakikisha wananunua mahindi kwa wakulima kwa shilingi 700 kwa kilo. “Vinginevyo, waende kununua mahindi NFRA moja kwa moja,” ameongeza Waziri Bashe.
Wakulima hao pia wameelezwa kuwa wataongezewa maghala ya kuhifadhi chakula, mizani ya kidigitali, kujengewa Kituo cha Zana za Kilimo, kupatiwa mbegu za mahindi za ruzuku zikiwemo aina ya Hybrid na OPV, pamoja na mbolea za ruzuku. Kuhusu miundombinu ya barabara na mawasiliano, Waziri Bashe ameeleza ataongea na viongozi wa sekta husika kwa ajili ya kusaidia ili kuongeza tija kwa wakulima.
Awali, Waziri Bashe alitembelea pia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed ambapo ameridhia ombi la Mkuu wa Mkoa kutumia shamba la Tumbaku la Ruvuma kuwa shamba la BBT kwa ajili ya matumizi ya wakulima waliopo karibu nalo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.