WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Maafisa Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali wanao wajibu wa kuhakikisha wanatoa taarifa za jinsi serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya kipindi cha miaka miwili imefanya.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha 18 cha Maafisa Mawasiliano na Uhusiano Serikalini (TAGCO) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam Machi 27, 2023
“Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini, mnao wajibu wa kuhakikisha mnatoa taarifa za jinsi serikali ilivyotatua shida hizo za wananchi kwani kwa kutofanya hivyo wapo watu wengine wataendelea kufanya upotoshaji wakati sisi wanahabari tunajua kuwa huo ni upotoshaji.”” Alifafanua.
Alisema jukumu la kuisemea serikali ni moja ya sehemu ya mawasiliano ya nje ya serikali kwahivyo wanapaswa kuzingatia.
Alisema sambamba na hilo, aliwataka wanahabari wote wa serikali na binafsi wahakikishe wananchi wanapata elimu na taarifa sahihi kuhusu faida na umuhimu wa miradi na mipango au shughuli zinazotelekezwa na serikali ikiwa ni pamoja na kuwapa taarifa sahihi kwa urahisi zaidi na kwa wakati.
Aidha aliwataka wazingatie suala la uhuru wa kupata na kutoa habari unaoendelea kutekelezwa kwa mujibu wa sheria, Taratibu na kanuni na wadau wote kila mmoja atimize wajibu wake.
Aliwataka kuimarisha matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuongeza upatikanaji wa habari kwenye maeneo yenu.“Kila mmoja kutoka mahali alipo, tunazo taasisi za mitandao ya kijamii ambazo zinafanya kazi pamoja na serikali, endeleeni kuwashirikisha katika kutoa taarifa za kazi na shughuli za serikali.” Alisisitiza.
Pia aliwataka kushiriki kikamilifu kuitangaza vema Tanzania ndani na nje ya nchi hususan sula la amani na utulivu, fursa za biashara na uwekezaji, historia ya nchi na kuweka msisitizo katika kufuata maadili na mila za nchi na kutangaza mali kale na vivutio
Aidha aliwataka kuweka mbele uzalendo, uadilifu, uhuru na maslahi ya nchi ili kulijenga taifa na aliwakumbusha kuongeza ubunifu wa kusukuma ajenda za serikali kwa umma.
Hali kadhalika aliwataka kujiendeleza ili kuendana na asi ya mabadiliko ya kiteknlojia.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye alisema Kikao hicho ambacho kimewaleta pamoja Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali kutoka Bara na Visiwani ni muhimu kwa ustawi na mchango wa kada hii katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za serikali.
“Kikao hichi kitatumika pamoja na mambo mengine kutathimini mchango wetu katika kusukuma ajenda mbalimbali za serikali na namna ya kuboresha mchango huo.” Alifafanua Mhe. Nnauye.
Katika hatua nyingine TAGCO kimempa tuzo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika kuimarisha sekta ya habari, demokrasia, uwazi, uhuru wa kutoa maoni na kupata taarifa nchini.
Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais.
Akikabidhi tuzo hiyo kwa niaba ya TAGCO, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye alisema, “Sisi maafisa habari serikalini, tumemwelewa, tunamwamini na tunamuunga mkono kwa dhati, Anaishi anayoyasema na anayatenda kwa ustadi mkubwa.” Alisema Mhe. Nape
Kauli mbiu ya Mwaka huu ni "Mawasiliano ya Kimkakati Injini ya Maendeleo".
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.