*YALIYOJIRI WAKATI WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS – TAMISEMI, MHE. INNOCENT BASHUNGWA AKIFUNGUA KIKAO KAZI CHA MAAFISA HABARI WA MIKOA, HALMASHAURI NA TAASISI ZAKE LEO JULAI 02, 2022 KATIKA UKUMBI WA OFISI YA MKUU WA MKOA WA DODOMA*
*Aliyosema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Innocent Bashungwa.
#Wakati wa kikao kazi cha 17 cha Maafisa Mawasiliano Serikalini kilichofanyika Mei 2022, Tanga, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye alitoa siku 14 kwa kila Taasisi kuhakikisha wamehuisha tovuti na mitandao yao ya kijamii lakini wengi wenu hamkufanya hivyo, sasa natoa siku 7 kwa Maafisa Habari wa Serikali kuhuisha tovuti hizo.
#Mpaka sasa ni Mikoa 11 tu ndio iliyowasilisha Taarifa za Uhuishaji wa Tovuti na mitandao ya kijamii hivyo naelekeza Maafisa Habari wa Mikoa 15 iliyobakia kuwasilisha Taarifa ndani ya siku tatu za kazi kuanzia Jumatatu Tarehe 04 Julai, 2022.
#Nimewaita hapa leo kuona Wizara, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Taasisi zake kwa pamoja, tunatimiza wajibu wetu muhimu, na wa lazima wa kuhabarisha umma juu ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita.
#Upelekaji wa habari kwa wananchi umekuwa ukisuasua kutokana na sababu mbalimbali ambazo nyingi zipo ndani ya uwezo wetu. Ninyi Maafisa Habari mnayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki yao ya msingi ya kupata taarifa.
#Shukrani nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha kada ya Maafisa Habari ambapo hapo awali kwenye Mikoa, Maafisa Habari walikuwa wako chini ya Idara ya Utawala na kwenye Halmashauri waliunganisha na Kitengo cha TEHAMA.
#Muundo mpya wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao umeanza kutekelezwa Julai 01, 2022, tumeanzisha Vitengo vya Mawasiliano Serikalini, vitasimamiwa na Wakuu wa Vitengo hivyo na kuwapatia fungu la fedha kwa ajili ya kujiendesha vyenyewe.
#Kwa Halmashauri ambazo zina Maafisa Habari wenye sifa zaidi ya mmoja, Ofisi ya Rais TAMISEMI itafanya msawazo, ili kwenda kujaza nafasi zilizopo wazi kwenye Halmashauri ambazo hazina Maafisa Habari kwa sasa.
#Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hakikisheni Maafisa Habari wanashiriki kikamilifu katika ziara zote za viongozi pamoja na Timu za Tathimini na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili waweze kuwa na uelewa wa kazi zinazofanywa na Mikoa na halmashauri.
#Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hakikisheni Maafisa Habari wanapatiwa mafunzo kazini kama vile uandishi wa takwimu (infographics/ data Journalism), vibango, kuhariri video na mafunzo mengine kadri itakavyoonekana inafaa.
#Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hakikisheni Maafisa Habari wanaingia kwenye Vikao vyote vya Kisheria ili kumuwezesha kuwa na uelewa mpana wa eneo lake la Kazi.
#Kila Afisa Habari aandae mpango kazi kutokana na Mpango Mkakati wa Taasisi husika na vipaumbele vya Taasisi ambavyo kwa ujumla vitasaidia Kuelimisha umma.
#Maafisa Habari muwasilishe taarifa ya utendaji kazi kila baada ya miezi mitatu kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mkoa ambaye naye ataziwasilisha kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano OR-TAMISEMI.
#Hakikisheni mnaandika habari zenye hamasa na kuibua ushuhuda kuhusu kazi za Serikali na miradi inayotekelezwa ambapo viongozi wa ngazi husika na Wananchi wa kawaida wahusishwe kuusemea mradi au kazi fulani zinazotekelezwa katika maeneo yao.
#Hakikisheni mnaandaa vipindi vya kutoa Elimu kwa Umma kupitia Vyombo vya Habari vya kijamii vilivyopo katika maeneo yenu na kuandaa ratiba kwa ajili ya Viongozi kushiriki kila wiki katika vipindi hivyo.
#Kila robo ya mwaka, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini OR - TAMISEMI awasilishe taarifa jumuishi ya Utendaji kazi wa Maafisa Habari wa Taasisi, Mikoa na Halmashauri, mafanikio na changamoto na kutoa ushauri kwa ambao ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao wachukuliwe hatua.
#Waajiriwa wote wapya wa kada za ualimu 9,800 na afya 6,876 wahakikishe wanaripoti kwa waajiri wao kabla au ifikapo tarehe 11 Julai, 2022 kama nilivyoelekeza awali nilipotangaza ajira hizo tarehe 26 Juni, 2022.
#OR – TAMISEMI haitambadilishia kituo mwajiriwa yeyote mpya aliyepangiwa kituo cha kazi katika ajira hizo kwa kuwa vituo walivyopangiwa ndivyo vyenye uhitaji kwa sasa.
#Wanafunzi wote waliopangiwa kujiunga na kidato cha tano, walipewa siku 14 za kuripoti shuleni hadi tarehe 30 Juni, 2022. Wale ambao hawajaripoti wafanye hivyo hadi tarehe 4 Julai, 2022 vinginevyo nafasi zao watapangiwa wanafunzi wa akiba.
#Wakuu wote wa shule wasiwatoze wanafunzi michango yoyote ambayo haijabainishwa kwenye miongozo na nyaraka za maelekezo ya Serikali. Mkuu wa shule yeyeyote atakayekiuka maelekezo haya atachukuliwa hatua stahiki.
#Nafasi 736 za kada ya Afya (madakari wa meno, mteknolojia mionzi, tabibu msaidizi na tabibu meno) zilizokosa waombaji wenye sifa zitatangazwa tena hivi karibuni.
#Napenda niwashukuru sana ninyi Maafisa Habari wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya katika kutangaza shughuli za Serikali.
*Aliyosema Kaimu Katibu Mkuu wa OR - TAMISEMI, Dkt. Charles Msonde*
#Ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kwamba wanafanya kila linalowezekana ili wananchi wapate taarifa sahihi na muhimu ambazo Serikali inawafanyia.
#Changamoto ni mchakato wa maendeleo, unapopata changamoto lazima uitafute fursa ya kutatua changamoto hiyo na tukishatatua changamoto tutakuwa tumepiga hatua kubwa ya maendeleo.
#Ninatambua kuwa Maafisa Habari mmepewa wajibu mkubwa sana wa kuhakikisha kuwa mnajitambua nyinyi wenyewe, mnafahamu na mnatekeleza majukumu yenu kwa weledi ili kuhakikisha kwamba haki ya mwananchi kupata habari inatimia.
*Aliyosema Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO, Gerson Msigwa.*
#Nawapongeza Maafisa Habari wote kwa juhudi mbalimbali mnazozifanya katika kutekeleza jukumu letu la kimawasiliano na kihabari katika kuiunganisha Serikali na Wananchi.
#Idara ya Habari imeweka utaratibu wa kuwa na mawasiliano na Maafisa Habari na kufanyia kazi changamoto hizo kupitia Idara na kupitia TAGCO. Nawaombeani tuendelee kutumia majukwaa haya.
#Naomba kuwasihi Maafisa Habari wenzangu kuwa tuchape kazi, kutangazwa kwa Mikoa, Wilaya na taasisi zetu kupo mikononi mwetu.
#Najua wengi watasema hawana bajeti, lakini sasa hivi kuna majukwaa ambayo hayatulazimu kulipia gharama za kutangaza taasisi zetu. Mitandao ya kijamii. Tuitumie kwa weledi.
#Nawatakia kazi njema na niwaombe tuendelee kuhamasisha Watanzania wote kujiandaa kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi iliyopangwa kufanyika tarehe 23 Agosti, 2022. Tukasimamie vyombo vya habari vilivyopo katika maeneo yetu hasa redio za kijamii vitangaze Sensa.
#Licha ya changamoto zilizopo, bado jukumu letu la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao halikwepeki kwa namna yoyote.
#Tunapaswa kuwa wabunifu na kubuni mikakati mipya ya kusemea maeneo yetu. Habari nyingi nchini zinapatikana katika Mikoa na Halmashauri zetu, tutumie vifaa tulivyonavyo kuhakikisha Wananchi wanapata taarifa.
#Nitoe wito kwenu kuzidi kutumia redio na televisheni za kijamii katika maeneo yenu kutangaza mafanikio na agenda za kitaifa kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaisaidia Serikali yetu kufikisha habari kwa wananchi na kuwawezesha kuwa na ufahamu wa yale yanayotekelezwa na Serikali yao.
*Aliyosema Afisa Habari Mkoa wa Dodoma, Sarah Kibonde*
#Tunamshukuru Rais wetu, Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kutujali Maafisa Habari kwa kuruhusu kuwa na vitengo vya habari vinavyojitegemea katika mikoa na wilaya.
#Kwa pamoja tunakuahidi kwamba tutatenda haki, tutafanya kazi kwa weledi na kuhakikisha lile jukumu la kutoa taarifa kwa Watanzania linatimia.
#Pia tutakuwa mstari wa mbele katika kutetea na kuhakikisha kwamba Serikali yetu haisemwi vibaya. Aidha, tunakuhakikishia Waziri Bashungwa kuwa tumepokea maelekezo yote na tutayafanyia kazi.
*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.