MAAFISA ugani wa Mkoa wa Ruvuma wamepewa mafunzo juu ya kanuni bora za kilimo cha Mkonge .
Mafuzo hayo yametolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania [TARI] Tanga katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa Ruvuma.
Mkuu wa mafunzo kutoka Taasisi ya Utafiti ya Kilimo Tanzania Frank Mabagala ameeleza umuhimu wa Mkonge kwa sasa kutokana na mabadiliko makubwa ya tabia ya nchi.
Amesema wakulima wamekua wakikosa mavuno kwa sababu hii TARI kwa kushirikiana na Bodi ya Mkonge Tanzania imeazimia kuhamasisha kilimo cha Mkonge kwa wakulima wadogo katika maeneo mbalimbali Tanzania ili zao litumike kwa kuwaleta tija kwa wananchi wa Tanzania.
Mtafiti Dietram Mkapa ameeleza umuhimu wa kilimo cha zao la Mkonge halina msimu maalumu wa kupanda na linapokuwa tayari kuvunwa kwa mwaka mara mbili ,hivyo ni zao ambalo linaweza kumpatia mkulima kipato cha uhakika katika kipindi chote cha mwaka.
Mkapa amesema Mkonge ni zao linalostahimili magonjwa na halidhuriwi kirahisi na magugu na majanga mengine kama moto,Pia ameongeza kuwa pembejeo kama mbolea,viuagugu na viuatilifu katika mazingira ya kawaida sio lazima kutumika ingawa matumizi yake yanaongeza uzalishaji wa mavuno ya mapema
Amesema zao la Mkonge linaweza kuchanganywa na mazao mengine kama kunde,maharage,mahindi,alizeti,njegere na karanga.
Mtafiti ameeleza matumizi ya Mkonge kuwa unaweza kutumika katika tasnia ya kilimo,nishati,ujenzi,famasia,magari,meli,majumbani,ofisini na mazingira mengine.
Mkapa amesema zao la Mkonge soko lake ni la uhakika hupatikana nje ya Nchi na ndani ya Nchi mmea wa Mkonge unaweza kuishi kwa kipindi cha miaka 10-25,hivyo kumuhakikishia mkulima kipato cha uhakika na kwa muda mrefu.
”Tubadili kilimo cha Mkonge kutoka uzio kuwa shamba la mkulima mdogo wa Mkonge, Halmahauri itumie zao la Mkonge kama zao mbadala katika maeneo makame na maeneo mengine yaliotelekezwa Pamoja na kutoa mafunzo kwa wakulima juu ya singa na ubora wa singa ,Halmashauri kwa kushirikiana na Bodi ianzishe vitalu mbegu bora za Mkonge katika maeneo makame”. amesema Mkapa.
Mkonge ni moja kati ya zao la biashara Tanzania,asili ya zao hili ni Mexico na baadae likasambaa katika nchi za India na Tanzania mwaka 1892, zao la Mkonge liliingizwa Nchini na mtaalamu wa kijerumani Dr.Richard Hindorff Ambaye alikua mtafiti wa mimea na udongo,Kutokana na mabadiliko ya hali ya uchumi nchini Tanzania serikali ya Tanzania ilipitisha sheria ya sekta ya mkonge ,1997;ambayo iliruhusu ubinafsishaji wa viwanda vinavyomilikiwa na serikali na kuanzisha Bodi ya Mkonge Tanzania.
Imeandaliwa na Bahati Nyoni
Kutoka Ofisi ya Habari ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Januari 27, 2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.