Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma Mhe. Peres Magiri, amekabidhi pikipiki mbili zilizonunuliwa na Serikali kupitia Mradi wa Maji wa Ngumbo awamu ya kwanza kwa vyombo viwili vya Watumia Maji: NGULIWSO cha Kata ya Ngumbo na Liwundi, na LILIMBAWSO cha Kata ya Lituhi, Linga, na Mbaha.
Makabidhiano hayo yalifanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, yakiwa yamehudhuriwa na wananchi, watumishi, na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.
Akikabidhi pikipiki hizo, Mhe. Magiri alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa Wilaya ya Nyasa pikipiki hizo pamoja na miradi ya maji ambayo imesaidia kutatua changamoto za wananchi. Aliwataka wanaopokea pikipiki hizo kuzitunza na kuzitumia kwa manufaa ya jamii, hususan kutatua changamoto za maji.
“Ninawakabidhi pikipiki hizi zikatumike vizuri kutatua changamoto kwa wananchi, ikiwemo kutengeneza mabomba maji yanapokatika. Zisitumike kubebea abiria au kwa manufaa binafsi. Tukibaini matumizi mabaya, hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” alisema Mhe. Magiri.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Masoud Samila,, alisema kuwa pikipiki hizo zitasaidia kuongeza usimamizi wa miradi ya maji. Alibainisha kuwa Wilaya ina vyombo nane vya watumia maji, lakini vitano kati ya hivyo havina usafiri.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi wa Jimbo la Nyasa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.