Katika Halmashauri za wilaya za Madaba, Mbinga, Tunduru, Songea na Namtumbo mkoani Ruvuma, mapinduzi ya kiuchumi yanaendelea kuota mizizi kupitia usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji, maarufu kama CBFM (Community-Based Forest Management).
Charles Meshack ni Mkurugenzi, TFCG akizungumza kwenye utambulisho wa mradi wa FORLAND mkoani Ruvuma anasema ni mageuzi yanayoweka jamii mbele katika usimamizi wa rasilimali, wakati huohuo yakiweka msingi wa maendeleo endelevu yanayoakisi dira ya Tanzania ya kijani.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023, zaidi ya shilingi bilioni 5 zilipatikana kupitia uvunaji endelevu wa mbao kutoka misitu inayosimamiwa na jamii mkoani Ruvuma na Lindi pekee. Fedha hizi zimeelekezwa katika huduma muhimu kama afya, elimu, miundombinu na usimamizi wa misitu, na kuonesha kuwa misitu ni chanzo cha matumaini.
Vijiji 26 Vyajitosa Rasmi Kuimarisha Misitu yao
Kupitia mradi wa kimataifa wa FORLAND unaogharimu zaidi ya Euro milioni 20.8, vijiji 26 katika Mkoa wa Ruvuma vimechaguliwa kushiriki kwa kina katika uanzishaji wa Hifadhi za Misitu ya Vijiji (VLFRs) na kupewa mafunzo maalum ya usimamizi wa misitu.
Mradi huu, unaofadhiliwa na Serikali ya Finland kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania, una lengo la kuimarisha uwezo wa jamii katika uzalishaji wa mbao, usimamizi wa moto, matumizi bora ya ardhi na kuibua fursa kwa biashara ndogondogo kupitia misitu.
Kwa sasa, asilimia 92 ya misitu kwenye ardhi ya vijiji haijalindwa, hali inayoonesha dharura ya kuongeza maeneo chini ya CBFM ili kukabiliana na ukataji hovyo wa misitu unaofikia hekta 600,000 kwa mwaka kitaifa.
FORLAND inalenga kubadilisha taswira hii kwa kutumia mbinu shirikishi, elimu, na teknolojia endelevu.
Misitu Inayozalisha Kipato: Mbao, Mkaa, na Kaboni
Mbali na mbao, baadhi ya vijiji mkoani Ruvuma sasa vimeanza kuzalisha mkaa endelevu kwa kutumia vitalu vya mzunguko wa miaka 24, na teknolojia za tanuri bora zinazolinda mazingira. Hii si tu inasaidia mazingira, bali pia inaleta mapato yanayotumika kulipia huduma za kijamii.
Mbali na hilo, miradi ya kimataifa kama REDD+ imeanza kulipa vijiji kwa kulinda misitu. Mfano wa kuigwa ni mradi wa Ntakata uliopatikana mapato ya USD milioni 5.7 kwa jamii mwaka 2023. Ruvuma, ikiwa na misitu mingi ya vijiji, ina nafasi kubwa ya kunufaika zaidi na miradi hii endapo vikwazo vya kisheria na kisera vitatatuliwa.
Misitu ni msingi wa uchumi wa vijiji
Wakati dunia inaendelea kuelekea kwenye uchumi wa kijani na uzalishaji endelevu, Ruvuma inajipambanua kuwa mfano hai wa mafanikio ya usimamizi wa misitu unaoongozwa na wananchi. FORLAND si mradi wa kupanda miti tu, bali ni mapinduzi ya fikra, sera na uongozi wa kijamii.
Akizungumza kwenye utambulisho wa mradi huo kwenye ukumbi wa Mipango Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Songea,Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Lous Chomboko ameupongeza mradi wa FORLAND kwa kudhamiria kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi vijijini kupitia mazao ya misitu.
Amesisitiza FORLAND wanapotekeleza mradi huo kuwashirikisha kikamilifu wananchi vijijini katika Halmashauri saba zinazoshiriki mradi huo katika Mkoa wa Ruvuma hali ambayo itawajengea uelewa wananchi na kuwekeza zaidi katika CBFM kama mkakati mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.