Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema Ruvuma ni kati ya mikoa 9 iliyokuwa na uibuaji mdogo wa wagonjwa wa kifua kikuu kwa mwaka 2024 ambapo wagonjwa 1,278 waliibuliwa kati ya lengo la wagonjwa 2,515 waliopaswa kuibuliwa.
Ameyasema hayo wakati akizindua Mpango Harakishi wa Kuibua Wagonjwa wa Kifua Kikuu uliofanyika katika uwanja wa nje ya soko kuu la Songea mjini lililopo manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
"Kwa Mkoa wa Ruvuma wagonjwa walioibuliwa ni asilimia 50.79 tu, hivyo bado tunalo jukumu la kuwapata wagonjwa 1,132 ambao bado wapo katika jamii tunayoishi wakiendelea kuwaambukiza watu wengine," alisema Kanali Ahmed.
Ameongeza kuwa takwimu zinadhihirisha kuwa ugonjwa wa kifua kikuu ni janga kubwa na kikwazo kwa maendeleo ya Taifa kwa sababu wanaougua wanashindwa kuzalisha mali hivyo kutochangia vizuri katika pato la Taifa na kumudu maisha yao wenyewe.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dr. Jacob Mwanamtwa, amebainisha kuwa kampeni hiyo ilianza Januari 20, 2025 na hadi kufikia Januari 22 wamefanikiwa kukusanya sampuli kwa wagonjwa 851 na waliogundulika kuwa na ugonjwa huo na kuanza matibabu ni 24 sawa na asilimia 2.8.
Amelitaja lengo la kampeni hiyo ni uharakishaji wa uibuaji wa wagonjwa wa kifua kikuu waliokosekana mwaka 2024 ili kuweka jitihada kwa pamoja na umoja katika kupambana na kifua kikuu, kuboresha na kuharakisha ufanisi wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kisare Makori, amesema kifua kikuu ni moja ya magonjwa yanayoambukizwa ambayo ni tishio hivyo wataendelea kushirikiana na viongozi mbalimbali wanaoratibu shughuli hiyo ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, amesema Tanzania ni moja kati ya nchi 30 zinazokabiliwa na tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu hivyo amewashauru wananchi wa wilaya wa Songea kukata bima ya Afya ili ziwasaidie hata wanapopata tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu wawe na uhakika wa kutibiwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2024 kulikuwa na wagonjwa milioni 10.8 wa kifua kikuu duniani kote, kati yao milioni 1.25 sawa na asilimia 12 walifariki kutokana na ugonjwa huo, Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya laki 122,000 sawa na wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000 walioibuliwa na kuanzishiwa dawa ni 92,720 sawa na asilimia 76.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.